Mwili wa Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mstaafu wa Mhe.
Samuel Sitta unatarajiwa kuwasili kesho Alhamisi Novemba 10, 2016 majira ya saa
9:00 alasiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere
Jijini Dar es Salaam.
Mwili huo unatarajiwa kupokelewa na Viongozi
Mbalimbali wa Kitaifa wa Chama na Serikali katika eneo la Terminal I.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa leo
Jijini Dar es Salaam na Ofisi ya Waziri Mkuu, mara baada ya kupokelewa katika
uwanja wa ndege, mwili huo utapelekwa nyumbani kwake Masaki jijini Dar es saam.
Aidha, taratibu za viongozi mbalimbali
na wanaombolezaji kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Marehemu Mhe.Sitta
zitafanyika katika Viwanja vya Karimjee siku ya Ijumaa ya tarehe 11
Novemba ,2016 kuanzia majira ya saa 1:30 asubuhi.
Mara baada ya
zoezi hilo kukamilika mwili wa Marehemu Sitta utapelekwa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa
Mwalimu Julius Nyerere kwa ajili ya kusafirishwa kuelekea
mkoani Dodoma siku ya Ijumaa tarehe 11 Novemba, 2016.
Mwili huo utawasili
mkoani Dodoma majira ya saa 8 mchana na kupokelewa na Viongozi mbalimbali wa
Mkoa wa Dodoma na Bunge.
Baadae mwili huo
utapelekwa katika Viwanja vya Bunge ambapo salamu mbalimbali zitatolewa na
Spika, Waziri Mkuu , Kambi Rasmi ya Upinzani na viongozi wa Mkoa wa Dodoma.
Mara baada ya kukamilika kwa zoezi
hilo, Waheshimiwa Wabunge na waombelezaji mbalimbali walioko katika Viwanja vya
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma watatoa heshima za mwisho
kwa mwili wa Marehemu na baadaye kupelekwa Uwanja wa Ndege wa Dodoma kwa ajili
ya kusafirishwa kwenda Urambo mkoani Tabora kwa ajili ya mazishi.
Mwili wa Marehemu Sitta unatarajiwa
kuwasili Uwanja wa Ndege wa Tabora majira ya saa 10 jioni ya 11 Novemba, 2016
na baadae kusafirishwa kuelekea nyumbani kwake Wilayani Urambo ambapo utawasili
majira ya saa 12 jioni.
Viongozi na waombezaji mbalimbali
Wilayani Urambo mkoani Tabora watatoa heshima za mwisho siku ya Jumamosi tarehe
12 Novemba, 2016 kuanzia asubuhi na mazishi yanatarajia kufanyika siku hiyo
hiyo majira saa 9 alasiri.
Marehemu Mhe. Sitta alizaliwa 18
Desemba, 1942 Urambo Mkoani Tabora
Imetolewa na Idara
ya Habari- Maelezo
9 Novemba, 2016
0 Comments