Mwenyekiti wa Bodi ya tiba asili na tiba mbadala Zanzibar Mohammed Kheri Mtumwa
akitoa tarifa ya kupiga marufuku matangazo na vipindi vinavyotolewa katika
vyombo vya habari alipokutana na wawakilishi wa vituo vinavyotoa huduma hiyo katika Wizara ya
Afya Zanzibar.
Baadhi ya wawakilishi wa vituo
vya tiba asili na tiba mbadala wakimsikiliza Mwenyekiti wao wa Bodi (hayupo
pichani) alipotangaza kupiga marufuku matangazo na vipindi vya huduma hizo
katika vyombo vya habari.
Sheikh Sabas Alkubra wa kituo cha tiba cha Jamaatul-Khairi akitoa mchango wake katika mkutano ulioitishwa
na Bodi ya Tiba asili na tiba mbadala katika Ofisi ya Wizara ya Afya Mnazi
mmoja Zanzibar.
Mrajisi wa tiba asili Haji Juma Haji akitoa ufafanuzi kuhusu kupigwa marufuku
matangazo ya tiba asili na tiba mbadala kwenye vyombo vya habari katika mkutano
uliofanyika Wizara ya Afya Zanzibar.
Picha na
Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar.
.............................................................................................
Na Ramadhani
Ali/Maelezo Zanzibar
Wizara ya
Afya kupitia Baraza la Tiba asili na tiba mbadala imepiga marufuku kwa mtu
yeyote kutoa huduma za tiba asili na tiba mbala bila ya kusajiliwa na Baraza
hilo.
Akizungumza na
wajumbe wa vituo vinavyotoa huduma hizo katika Wizara ya Afya Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la tiba asili na tiba
mbadala Mohammed Kheri Mtumwa amesema kuanzia sasa hairuhusiwi kuendesha kituo
cha kutolea huduma za tiba asili au tiba mbadala bila kusajiliwa.
Amewaeleza
wajumbe hao kuwa ni marufuku kuuza au kugawa dawa ya tiba asili ama tiba
mbadala mpaka iwe imesajiliwa na kufanyiwa uchunguzi na maabara ya mkemia mkuu
wa Serikali na kupewa kibali na Bodi ya Chakula Dawa na Vipodozi.
“Wizara
inapiga marufuku kwa mtu binafsi au taasisi yoyote kutumia kifaa tiba chochote
bila kusajiliwa katika sehemu husika ya usajili wa vifaa tiba,”alisisitiza
Mwenyekiti wa Baraza.
Ameongeza kuwa
matangazo yote na vipindi vinavyohusu
tiba asili na tiba mbadala ambayo hayajapitishwa na Baraza yamezuiliwa kuanzia
sasa.
Amesema lengo
la Wizara kupitia Baraza la tiba asili na tiba mbadala kuweka masharti ya kutoa huduma hizo ni kutaka kuhakikisha
sheria, kanuni na miongozo inayotolewa inafuatwa.
Amesema Serikali
inatambua na inathamini huduma za tiba asili na tiba mbadala na ni huduma
inayotambuliwa na sayansi ya tiba ya kisasa lakini kwa muda mrefu imekuwa
ikiendeshwa kama haina msimamizi.
Mwenyekiti huyo wa Baraza amewaeleza wajumbe hao kuwa
iwapo wataongeza mashirikiano na kuboresha huduma za tiba asili wataweza kuuza dawa na huduma hizo nje ya nchi
na kuimarisha uchumi wa nchi.
Nao wajumbe
kutoka vituo vya tiba asili na tiba mbadala wameishauri Wizara ya Afya kupitia Baraza
lao kuwajengea mazingira mazuri yatakayowawezesha kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.
Wamesema suala
la kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali za kutoa huduma za tiba asili na tiba mbadala siyo tatizo
kwani wanafahamu kila jambo linataratibu zake katika kuliendesha.




0 Comments