Random Posts

SERIKALI YA TANZANIA KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA JAPANI KATIKA KULETA MAENDELEO NCHINI

 Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Naibu Balozi Msafiri Marwa akizungumza na Wataalam wa Kujitolea kutoka Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japani (JICA) (hawapo pichani) katika hafla fupi ya kuwakaribisha Wataalam hao ambao watafanya kazi katika maeneo mbalimbali nchini kwenye sekta za Elimu, Afya na Maendeleo ya Jamii, hafla iliyofanyika Ofisi ya Rais-Utumishi mapema leo,
 Mratibu wa Wataalam wa Kujitolea kutoka Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japani (JICA), Bw. Mada Hideki akifafanua jambo kwa Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Naibu Balozi Msafiri Marwa (hayupo pichani) katika hafla fupi ya kuwakaribisha Wataalam saba wa kujitolea iliyofanyika Ofisi ya Rais-Utumishi mapema leo.
 Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Naibu Balozi Msafiri Marwa akimsikiliza Mratibu wa Wataalam wa Kujitolea kutoka Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japani (JICA), Bw. Mada Hideki katika hafla fupi ya kuwakaribisha Wataalam saba wa kujitolea iliyofanyika Ofisi ya Rais-Utumishi mapema leo.
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Naibu Balozi Msafiri Marwa akiagana na Wataalam wa Kujitolea kutoka Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japani (JICA) mara baada ya hafla fupi ya kuwakaribisha Wataalam hao ambao watafanya kazi katika maeneo mbalimbali nchini kwenye sekta za Elimu, Afya na Maendeleo ya Jamii.
....................................................................................
Serikali ya Tanzania imeihakikishia Serikali ya Japani kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japani (JICA) kuwa itaendelea kutoa ushirikiano kwa nchi hiyo ili kuleta maendeleo endelevu katika sekta mbalimbali nchini ikiwemo afya, elimu na maendeleo ya jamii.

Hayo yalisemwa na Kaimu  Katibu Mkuu , Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma,  Naibu Balozi Msafiri Marwa wakati wa hafla fupi ya kuwakaribisha watalaam saba ( 7) wa kujitolea kutoka  nchini Japani iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Rais-Utumishi mapema leo.

Kaimu Katibu Mkuu alisema Tanzania itaendelea  kudumisha ushirikiano huo  na Japani  ili kuendelea kunufaika hasa katika suala zima la kujengewa uwezo katika sekta hizo ambazo pia  zimepewa kipaumbele  katika Awamu ya Pili ya  Mpango wa Serikali wa  miaka Mitano (5) wa Maendeleo inayoanza mwaka 2016/17 na kumalizika mwaka 2021/22.

Alisema tangu mwaka 1967 hadi sasa vijana wa Japani 1,542 wameshafika nchini na kufanya kazi za kujitolea katika maeneo mbalimbali hata katika mazingira magumu.

“Pamoja na kunufaika katika sekta za elimu, afya na maendeleo ya jamii, ushirikiano huo pia unatupa nafasi ya kubadilishana uzoefu katika kuelewa tamaduni za nchi hizi mbili,” Naibu Balozi Marwa alisema.

Kwa upande wake, Mratibu wa Wataalam wa Kujitolea kutoka Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japani (JICA), Bw. Mada Hideki aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano ambao imekuwa ikiutoa kwa Serikali yao na hivyo kuwawezesha wataalam wa kujitolea kuweza kufanya kazi waliyoikusudia.

Wataalam hao ambao wako saba (7) watafanyakazi ya kujitolea katika sekta ya elimu, afya na maendeleo ya jamii kwa miaka miwili katika mikoa ya Mwanza, Iringa na Mtwara.

Post a Comment

0 Comments