.............................................................................................................
Na
Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma.
Mwili
wa aliyekuwa Spika wa Bunge la 9 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samuel
Sitta unatarajiwa kuagwa leo mchana na wabunge wa Bunge hilo katika viwanja vya
Bunge vya mjini Dodoma.
Kauli
hiyo imetolewa mjini hapo na Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai alipokuwa akitoa
ratiba ya kuuaga mwili wa spika mstaafu itakayoanza mara baada ya kumalizika
kwa shughuli za Bunge za kipindi cha asubuhi.
Mhe.
Ndugai amesema kuwa Bunge linatarajia kuupokea mwili wa mpendwa huyo leo mnamo
majira ya saa 8 mchana kutoka katika uwanja wa ndege wa Dodoma na kupelekwa
moja kwa moja ndani ya Bunge hilo kwa ajili ya kupewa heshima za mwisho na
wabunge.
“Baada
ya mwili wa mpendwa wetu kuwasili katika viwanja hivi, tutakuwa na kikao maalum
cha Bunge kitakachofanyika mida ya saa 8:30 mchana ambapo wabunge watapata
nafasi ya kutoa salamu za rambirambi na baadaye utaratibu wa kutoa heshima za
mwisho utafuata”, alisema Mhe. Ndugai.
Spika
Ndugai ameongeza kuwa baada ya utoaji wa heshima za mwisho utakaoongozwa na
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa pamoja na Kiongozi wa Kambi rasmi ya
Upinzani Bungeni Mhe. Freeman Mbowe, kwa mwili wa marehemu Samuel Sitta utasafirishwa
kwa ndege mnamo majira ya saa 10 jioni kwenda wilaya ya Urambo, mkoani Tabora
kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika Novemba 12 mwaka huu.
Aidha,
Mhe. Ndugai amefafanua kuwa katika msiba huo Bunge litawakilishwa na wabunge 10
watakaochaguliwa na Tume ya Huduma za Bunge kwa kuzingatia uwakilishi wa vyama
ukiongozwa na yeye Spika Mhe. Ndugai kwenda mkoani Tabora kwa ajili ya mazishi.
Kutokana
na msiba huo, Mhe. Ndugai amesema kuwa Bunge litajenga misingi ya kuwaheshimu
viongozi wa kitaifa wanaopatwa na jambo la namna hiyo kwa kupewa heshima hizo
za kuletwa Bungeni kwa ajili ya kuagwa kwa msingi wa Bunge kuwa ndio nyumba ya
uwakilishi wa Watanzania wote.

0 Comments