Na Daudi Manongi, MAELEZO
Kampuni
ya Reli Tanzania (TRL) imekusanya shilingi bilioni 8.1 katika robo ya kwanza ya
mwaka 2016 ikiwa ni zaidi ya shilingi bilioni 1.6 ya robo ya kwanza ya mwaka
2015 ambapo ilipata mapato ya zaidi ya shilingi bilioni 6.5.
Hayo
yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TRL Bw.Masanja Kungu Kadogosa wakati akiongea
na waandishi wa habari ofisini kwake Jijini Dar es Salaam.
Bwana
Masanja anasema kuwa huduma ya usafirishaji abiria imezalisha mapato ya wastani
wa shilingi bilioni 1.1 katika kipindi cha mwaka 2016 na Wastani wa shehena kwa robo mwaka imeongezeka na kufikia
tani 63,251 ukilinganishwa na tani 48,681 zilizosafirishwa katika kipindi kama
hicho mwaka jana.
Aidha
kati ya mwezi Juni hadi Octoba mwaka 2016 kampuni imetekeleza miradi midogo
kadhaa ya kujenga michepuo ya reli kwenda kwenye viwanda vya wateja wa TRL
wenye kuzalisha shehena,ambapo Baadhi ya miradi ya reli za michepuo
zilizojengwa ni kwenda kiwanda cha mbolea cha Yara kilichopo Kurasini na kiluwa Group ya Mlandizi
huku michepuo mingine inatarajiwa kujengwa kuelekea viwanda vya Saruji vya
Rhino na Sungura vilivyopo mkoani Tanga.
Aidha
Bw.Kadogosa amesema kuwa wamefanikiwa kufanya ukarabati wa mabehewa ya mizigo
120 yaliyogharimu shilingi milioni 700 na kusema kama yangefanyiwa ukarabati
nje ya nchi yangegharimu shilingi bilioni 26.
Mbali
na hayo menejimenti ya TRL inaendelea kutoa kipaumbele katika kutatua madai ya
wafanyakazi wake ikiwemo kuwasilisha Michango katika mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF),WADU
na Saccos NMB ambapo baada ya kuwasilisha makato wafanyakazi wameanza kupata
huduma stahiki.
Aidha
malimbikizo ya nyongeza ya mshahara yameshatengewa shilingi milioni 600 ambazo
zimelipwa ikiwa ni awamu ya tatu na menejimenti inajipanga kumaliza awamu
nyingine zilizosalia.
Mkurugenzi
huyo ametoa wito kwa wadau na wananchi kuhakikisha wanalinda miundombinu ya
reli na kuripoti mara moja kwenye vyombo vya dola wale wote wanaohujumu
miundombinu kwa manufaa binafsi.

0 Comments