Kamanda wa kitengo cha usalama barabarani mkoani Pwani, Abdi Issango pichani.
(Picha na Mwamvua Mwinyi)
.................................................................................................................
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
WATUNGA sera kupitia serikalini wameombwa kuangalia uwezekano wa kuzifanyia marekebisho baadhi ya sheria za usalama barabarani ikiwemo adhabu za faini zinazotolewa ziweze kuwa na maumivu kwa wakiukwaji.
Watunga sera hao wanatakiwa kuzipitia upya sheria hizo (The road traffic act cap 168) ya mwaka 1973 kwani kifungu cha 50 kulipita gari vibaya adhabu yake ni sh 1,000 na isizidi 2,000 na kifungu cha 45 dereva aliyekutwa amelewa ni sh.10,000 hadi 20,000.
Kamanda wa usalama barabarani mkoani Pwani, Abdi Issango ,aliyasema hayo wakati akizungumza na wadau wa usalama barabarani na waandishi wa habari.
Alisema baadhi ya sheria ni za zamani hivyo zinapaswa kwenda na wakati na haina budi ziangaliwe upya kwa kubadilishwa ili kwenda na hali ilivyo sasa.
Kamanda Issango alieleza kwamba sheria hizo husababisha baadhi ya watumiaji barabara hususan madereva kutokuwa na hofu ya kukiuka sheria kutokana na faini kuwa ndogo.
“Mfano wa sheria ya usalama barabarani (The Road Traffic Act Cap 168) ya mwaka 1973 adhabu nyingi ni ndogo na hazileti majuto wala hofu kwa mkosaji , ni kinyume na malengo ya adhabu ya kumpa maumivu mhusika”
“Kifungu cha 50 cha kulipita gari jingine vibaya adhabu yake ni sh. 1,000 na isizidi sh.2,000 na kifungu cha 45 dereva akitiwa hatiani kwa kosa la ulevi adhabu yake ni sh.10,000 na isizidi 20,000,” alisema Issango.
Alifafanua adhabu inatakiwa mkosaji apate majuto,hofu na maumivu ili ajutie kosa na kuogopa kosa alilotenda, hivyo kutokana na adhabu hizo kuna haja ya kuzipitia upya sheria hizo ili zitoe adhabu kali.
Issango ambae pia ni katibu wa kamati ya usalama barabarani mkoani hapo alitoa rai kwa jamii na wadau mbalimbali kuipigia kelele serikali ili iweze kubadilisha baadhi ya vifungu vinavyotoa adhabu ndogo kwa wakosaji .
Alieleza endapo adhabu zitakuwa kubwa itasababisha kuogopa ama kusita kurudia makosa kwa makusudi kwani wengine wanarudia kwa kujua adhabu siyo kali.
Issango alisema katika kukabiliana na ajali mahakama zinapaswa kutenda haki na kumaliza kwa wakati kesi zinazotokana na usalama barabarani .
Alisema pia wadau wote wanapaswa kushirikiana ili kupunguza ajali ambazo nyingine zimekuwa zikisababishwa kutokana na uzembe.
“Nawasihi madereva wa vyombo vyote vya moto kuacha kufanya mbwembwe wakiwa barabarani ,kutotumia vilevi wakati wakiendesha ,kuacha kupita magari mengine(overtake)ovyo na mwendo kasi ili kuepukana na ajali”anasisitiza .

0 Comments