Mzee wa Kanisa kutoka Jumuiya ya Maili Moja A ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT Usharika wa Maili Moja, Samwel Luhembe kushoto akikabidhi sabuni kwa ajili ya familia ya watu saba wasioona Mwajuma Maulid.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maili Moja A ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT usharika wa Maili Moja Jacob Samson kushoto akimkabidhi moja ya msaada uliotolewa na Jumuiya hiyo kwa family ya watu saba wasioona anayepokea ni Mwajuma Maulid ambaye ndiye mama anayeihudumia familia hiyo.
Mzee wa Kanisa kutoka Jumuiya ya Maili Moja A Samwel Luhembe kushoto akikabidhi unga uliotolewa na jumuiya hiyo ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT usharika wa Maili Moja anayepokea ni mama wa familia ya watu wasioona saba Mwajuma Maulid kulia.
Baadhi ya wanafamilia wasioona wakiwa kwenye picha ya pamoja.
(Picha zote na Mwamvua Mwinyi)
..........................................................................................................................
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
JUMUIYA ya Maili Moja A ya kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT) ,usharika wa Maili Moja, imetoa misaada ya nguo na vyakula kwa familia yenye watu saba ,wenye ulemavu wa kutoona inayoishi ,mtaa wa Simbani wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Misaada hiyo imetolewa kwa lengo la kuwezesha familia hiyo nayo iweze kusheherekea sikukuu za mwisho wa mwaka .
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa kwa misaada hiyo, mwenyekiti wa jumuiya ,Jacob Samson alisema ,wameguswa bada ya kupata taarifa za hali ya familia hiyo.
“Familia hii inamahitaji mbalimbali ,mbali ya hivyo sikukuu kama hizi nao wanataka kufurahi kwa kula na kuvaa kama wengine,tunaamini kusaidia jamii zenye mahitaji ni ibada kamili na inawatia moyo na kujiona kuwa hawako peke yao”alisema Samson.
Samson alieleza kwamba jumiya hiyo huwa ikifanya ibada za nyumba kwa nyumba ambapo hutembeleana na kushirikiana kwenye masuala mbalimbali ya kijamii na kiimani.
“Wanajumuiya walisema tuje kuifariji familia hii,ili iwe sehemu ya ibada yetu na kuitia furaha familia hii kwenye kipindi hiki cha mwisho wa mwaka,” alisema Samson.
Hata hivyo aliiomba jamii ijitokeze kuisaidia familia hiyo ambayo inahitaji misaada mbalimbali kutokana na kuwa kwenye mazingira magumu.
“Kutoa ni moyo na si utajiri kwani watu wenye moyo wanapaswa kwenda kuwasaidia kwa jambo lolote la kijamii hasa ikizingatiwa familia hiyo inasimamiwa na mwanamke ambae alitengana na mumewe,” alisema Samson.
Nae mama wa familia hiyo Mwajuma Maulid ,aliishukuru jumuiya ya Maili Moja kwa kuwapatia misaada hiyo .
Alieleza vyakula vilivyotolewa vitawasaidia katika kusherehekea sikukuu ya X-Mass kwa furaha kama wanavyofurahia watu wengine na kuwaomba watu wengine waendelee kuwasaidia.
“Tuko kwenye mazingira magumu ,tunaishi maisha ya kubahatisha kwa hiyo wanapokuja watu tunafarijika na kushukuru kwa kile wanachotupatia,” alisema Mwajuma.
Familia hiyo inaishi kwa kutegemea kuchoma mkaa na kusuka mikeka,ina watu saba ambao hawaoni akiwemo mume wake ambae walitengana,watoto wanne wasioona na wajukuu wawili.
No comments:
Post a Comment