WINGA wa kushoto wa Klabu Bingwa
ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Farid Mussa, ameweka wazi kuwa mabingwa
hao hawajambania kwenda nchini Hispania kucheza soka la kulipwa kama
ilivyoripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari.
Kwa kuudhihirishia umma, Mussa
leo amejitokeza hadharani na kupinga madai hayo akidai kuwa muda wowote kuanzia
sasa atakwenda nchini humo kujiunga na Club Deportivo Tenerife inayoshiriki
Ligi Daraja la Kwanza baada ya kupata ‘Visa’ maalumu ya kuingia nchini akiwa
kama mfanyakazi.
“Kwanza napenda kumshukuru Mungu
baada ya kupata visa, haikuwa kazi rahisi namshukuru Meneja Mkuu Abdul
(Mohamed) kapigania hadi suala hili limekamilika, cha kwanza nilikuwa
ninawaomba Watanzania wajue kuwa Azam haikuwa inanibania ni masuala tu ya visa
yalikuwa yakisumbua ubalozini.
“Mara baada ya kupata visa ya
kufanya kazi muda wowote ninaweza kuondoka kuanzia Januari,” alisema Farid
wakati akizungumza mbele ya waandishi wa habari leo wakati wa zoezi la
kutambulishwa wachezaji wapya waliosajiliwa na timu hiyo.
Taarifa hizo zilianza kutolewa
kwenye vyombo vya habari, kufuatia suala la Farid kwenda Hispania kuwa kimya
lakini ukweli wa mambo ni kuwa visa hiyo ndio iliyokuwa ikikwamisha dili hilo.
Naye Ofisa Habari wa Azam FC,
Jaffar Idd, akitolea ufafanuzi suala hilo alisema kuwa lengo la uongozi huo
lilikuwa ni kinda huyo kuondoka mapema kuelekea nchini humo, lakini suala kubwa
lilikwamisha ni visa hiyo ya kufanya kazi nchini Hispania.
“Uongozi wa Azam FC ulikuwa
sambamba na Tenerife kuhakikisha Farid anaondoka, lakini tunashukuru suala hilo
limekamilika kwa asilimia 98, lakini ni kwamba Farid muda wowote kuanzia sasa
Mungu akijaalia ndani ya wiki mbili zijazo au wiki moja anaweza kuondoka kutoka
Tanzania kuelekea Hispania,” alisema.
Azam FC inaamini ya kuwa kuondoka
kwa nyota huyo wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kutafungua milango
kwa wachezaji wengine ndani ya timu hiyo na Taifa kwa ujumla kuweza kupata
nafasi ya kucheza soka la kulipwa barani Ulaya.

0 Comments