Kamanda wa kitengo cha Usalama Barabarani mkoani Pwani, Abdi Issango.
(Picha na Mwamvua Mwinyi)
....................................................................................................................................
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
JESHI la polisi mkoani Pwani kitengo cha usalama barabarani kinatarajia kuanza ukaguzi wa magari mabovu na kuwapima madereva macho, presha na kiwango cha ulevi ili kudhibiti ajali katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.
Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani hapo, Abdi Issango alisema zoezi hilo limeshaanza mwishoni mwa wiki ambapo wanalifanya kwa kushikiana na SUMATRA, wadau wa afya, jeshi la zima moto na bima.
Alisema lengo hasa ni kuhakikisha katika msimu huu wanadhibiti na kuwa endapo dereva yeyote atakutwa na makosa yanayoashiria kusababisha ajali atapelekwa mahakamani ama kutozwa faini .
Issango ameeleza kuwa madereva watakaobainika kuwa na matatizo ya macho ama presha watazuiliwa kuendelea na safari.
"Tutawakamata, kuwatoza faini na kuwapeleka mahakamani madereva wote watakaokutwa na makosa mbalimbali hasa hatarishi ikiwemo ulevi, kuzidisha abiria, mwendokasi , hadi hapo watakapojirekebisha", alisema Issango .
Akizungumzia hali ya ajali katika mkoa wa Pwani Issango alisema ajali zimepungua hasa zinazohusisha magari makubwa ya abiria na sasa ajali zinazoongoza ni zinazosababishwa na pikipiki na magari madogo.
“Katika wilaya ya kibaha pekee ndio kunatokea ajali kwa asilimia kidogo, lakini hii inatokana na ufinyu wa barabara ya Morogoro, tumeiomba serikali itusaidie kupanua barabara hii ambayo ndio chanzo kikuu cha ajali katika mkoa wetu”, alisema Issango.
Hata hivyo Issango amewapongeza wadau mbalimbali wa barabara na madereva kwa ushirikiano wao wa kupokea elimu ya usalama barabarani na kuchangia kupunguza ajali.
Issango alieleza kwamba katika kipindi cha mwaka 2016/2017 kitengo hicho kimejipanga kumaliza tatizo la ajali.
Alisema kwa kipindi cha januari hadi septemba 2016,watu 165 wamekufa kutokana na ajali za barabarani ambapo vifo hivyo ni pungufu ya watu 18 ikilinganishwa na vifo vya ajali katika kipindi kama hicho mwaka 2015.
“Madereva waliokufa walikuwa 27 ikiwa ni ongezeko la madereva 14 ikilinganishwa na waliokufa kipindi kama hicho walikuwa 13 ongezeko likiwa ni asilimia 107.6 ,abiria waliokufa walikuwa 36 pungufu ikiwa ni vifo 39 sawa na asilimia 52 wapanda baiskeli vifo vilikuwa 13 ongezeko la vifo 11,” alisema Issango.

0 Comments