Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Mhe. William Lukuvi akisalimiana na Maafisa wa Serikali mkoani Shinyanga
mara baada ya kuwasili katika wilaya hiyo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya
Shinyanga Josephine Matiro.
Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wakiwa
katika foleni ya kukabidhi malalamiko yao ya migogoro ya ardhi na bahasha za
kero za ardhi kwa Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ili atolee
ufumbuzi.
Bahasha zaidi ya mia mbili (200) za kero
za migogoro ya ardhi zikiwa zimepokelewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ili aitatue.
Wananchi
wa Mkoa wa Shinyanga wakiandika maelezo kuhusu matatizo wanayokumbana nayo katika
umiliki wa ardhi mkoani Shinyanga ili Waziri wa Ardhi ayatatue.
Wananchi
wa Mkoa wa Shinyanga wakiwa eneo la mkutano wakisubiri zamu ya kueleza kero za
ardhi kwa waziri.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Mhe. William Lukuvi akitatua mgogoro wa ardhi wa Bibi Safina Ibrahim
mara baada ya kuleta vielelezo vyake.
Msafara wa Waziri wa Ardhi, ukiwa umewasili
katika jengo la Halmashauri ya wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga kwa ajili ya
kukutana na wakuu wa idara hususani wa sekta ya ardhi wa Kishapu kabla ya
kwenda katika mkutano wa kusikiliza kero za wananchi katika mji wa Mhunze.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi Mhe. William Lukuvi akimkabidhi vitabu vyenye muongozo namna ya
kupanga miji sambamba na kitabu chenye majina 33 ya makampuni yaliyojitolea
kushirikiana na serikali kupima ardhi.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi Mhe. William Lukuvi akitatua mgogoro wa ardhi wa wananchi wa Kishapu
waliokuwa wanagombea eneo la makazi.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi Mhe. William Lukuvi akimhoji Mthamini wa wilaya ya Kishapu Reuben Lauwo
(mwenye shati ya bluu) na Afisa Ardhi wa wilaya ya Kishapu Grace Pius (gauni la
kitenge) kwanini hawakumlipa fidia bwana Daudi Amos (wa kwanza kushoto) kama
inavyostahiki.
.......................................................................................................
Na. Hassan Mabuye (Kitengo cha Mawasiliano - Wizara ya Ardhi)
Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo
ya Makazi Mhe. William Lukuvi amekutana wakazi wa Shinyanga na kusikiliza kero
zao za ardhi na kuzitatua ambapo wananchi walijitoka kwa wingi katika viwanja
vya Zimamoto Nguzo Nane mjini Shinyanga ambapo
Waziri Lukuvi amepokea kero zaidi ya
200 za ardhi mkoani Shinyanga zinazodaiwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na
maafisa ardhi,wenyeviti wa mitaa waliojikuta wakishindwa kujibu kero hizo mbele
ya waziri huyo.
Waziri Lukuvi alisema baada ya
kupokea kero hizo ataunda kikosi maalum cha wataalam watakaoweka kambi mkoani
Shinyanga kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi na wataitwa mmoja mmoja
kisha kujibiwa kwa maandishi.
“Kama mmekaa na kero za ardhi tangu
mwaka 2008 mpaka leo,naomba mniamini basi mimi kwa sababu Waziri ndiyo mwenye
majibu ya mwisho kuhusu kero zenu,nilichobaini viongozi hawasikilizi kero za
wananchi, kuna kero zingine hazikupaswa kuletwa kwangu mngemalizana huko
huko”,alieleza Waziri Lukuvi.
“Kama kuna maafisa ardhi wamekuwa
sehemu ya migogoro ya ardhi lazima wawajibishwe,haiwezekani wananchi waichukie
serikali kwa sababu ya watendaji wasio waaminifu,kiongozi atayebainika
kuigombanisha serikali na wananchi tutaachana naye”,aliongeza Lukuvi.
Waziri Lukuvi ametoa wito kwa
wananchi wenye kero za ardhi wanapotoa ushahidi wawataje kwa majina watu wote
waliohusika katika kukuza migogoro ya ardhi na kusababisha wananchi
kunung’unika kwa kukosa haki zao ili waweze kuchukuliwa hatua.
Kufuatia udhaifu huo aliwataka
viongozi akiwemo Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri
kupanga muda wa kusikiliza kero za wananchi ili kupunguza kero za wananchi.
Wakizungumza mbele ya waziri
huyo,wananchi walisema baadhi ya watendaji wa serikali,wenyeviti wa mitaa na
maafisa ardhi wamekuwa chanzo kikubwa cha migogoro kwa kuendekeza rushwa na
kujuana.
Mheshimiwa William Lukuvi akiwa
wilani kishapu Mkoani Shinyanga ameendelea na ziara ya kusikiliza kero za
wananchi kuhusu masuala ya ardhi na kuzitatua.
Akizungumza katika viwanja vya
Ushirika katika mji wa Mhunze wilayani Kishapu wenye kata 25,vijiji 117 na
vitongoji 660 wakati akisikiliza kero za ardhi kutoka kwa mwananchi mmoja baada
ya mwingine,Waziri Lukuvi alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais
John Pombe Magufuli imedhamiria kumaliza kero za ardhi.
Ziara hiyo imekuwa na manufaa kwa
wakazi wa Kishapu baada ya waziri huyo kuahidi kuanzisha baraza la ardhi katika
wilaya hiyo hivi karibuni na wiki ijayo atateua mwenyekiti wa Baraza hilo ili
kutatua kero za ardhi na kuwapunguzia wananchi adha ya kusafiri umbali mrefu
kufuata huduma hiyo katika wilaya ya Shinyanga.
Lukuvi aliwataka maafisa wa ardhi
nchini kushirikiana na sekta binafsi kupanga miji na wao kubakia kuwa
wasimamizi wa taratibu zote kwani serikali haina uwezo wa kuajiri maafisa ardhi
na mipango miji wengi.
Waziri Lukuvi pia amepiga marufuku
vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wawekezaji wasio waaminifu waliopewa vibali
vya kuchimba madini kuwahamisha wananchi katika maeneo ya uchimbaji bila
kuwalipa fidia.
“Kama umepewa kibali na serikali cha
kuendeleza eneo flani la mgodi wale wananchi wa pale lazima waondoke lakini
waondolewe kwa heshima, wapewe fidia inayofanana na thamani ya mali zao
zilizopo eneo lenye mgodi siyo fidia ya kupunza wananchi kama kulikuwa kuna
nyumba wajengee nyumba zingine nzuri ndio uwaamishe”,alisema Lukuvi.
0 Comments