WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
hadi kufikia sasa, Serikali imekwishaipatia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto sh. bilioni 40
kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba.
Amesema hatua hiyo inalenga
kupunguza changamoto ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba iliyokuwa inazikabili
hospitali mbalimbali nchini.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
(Alhamisi, Desemba Mosi, 2016) wakati akizungumza na viongozi wa Mkoa wa
Manyara aliposimama wilayani Babati akiwa njiani kwenda Mkoani Arusha kwa ziara
ya kikazi ya siku saba inayotarajiwa kuanza kesho.
Amesema suala la dawa kwa sasa
linaenda vizuri, hivyo amewataka viongozi wa mikoa kuhakikisha dawa na vifaa
tiba vinavyopelekwa katika hospitali zao zinatumika kama ilivyokusudiwa.
“Suala la dawa linaenda vizuri sasa.
Hakikisheni mnadhibiti mianya ya upotevu wa dawa kwenye hospitali zetu kwa
kuwachukulia hatua za kisheria watumishi wa sekta ya afya wasiokuwa waaminifu,”
amesema.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka
viongozi hao kuweka utaratibu wa kujenga hospitali ya rufaa ya mkoa pamoja na
kuhamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili kuwawezesha
kupata huduma ya matibabu bure kwa mwaka mzima.
Wakati huo huo, Waziri
Mkuu amewataka viongozi hao kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuachana na mila
potofu na badala yake wawasomeshe watoto wao hasa wa kike kwani suala la elimu
mkoani Manyara bado halijapewa kipaumbele.
“Hakikisheni watoto wote waliofaulu
kwenda kidato cha kwanza wanakwenda shule ifikapo Januari. Maofisa Elimu
shirikianeni na halmashauri kuhakikisha jambo hili linafanikiwa kwaasilimia 100,”
amesema.
Akizungumzia kuhusu suala la utoro
na mimba kwa watoto wa kike, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao kudhibiti jambo
hilo kwa kuwachukulia hatua za kisheria wazazi na walezi wa wanafunzi hao.

0 Comments