Kaimu Katibu Mtendaji kutoka Tume ya Mipango,
Bibi Florence Mwanri (aliyevaa suti) akiwa pamoja na maofisa wa mamlaka ya
viwanja vya ndege na wa Tume ya Mipango wakielekea kukagua maeneo mbalimbali ya
kiwanja hicho.
Sehemu ya barabara inayotumika katika kutua
na kuruka ndege (Runway) ya Kiwanja cha Mtwara. Urefu wa barabara hiyo ni mita 2258
na ina upana wa mita 30.
Meneja wa Teknolojia na Mawasiliano kutoka
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini , Bw. Abdulatif Min-Hajj (aliyekaa kulia kwa Kaimu Katibu Mtendaji) akielezea
mpango wa kuboresha kiwanja cha ndege Mtwara mbele ya timu ya Ukaguzi wa Miradi
ya Maendeleo kutoka Tume ya Mipango.
Kaimu Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango Bibi
Florence Mwanri akitoa ushauri kwa
maofisa wa mamlaka ya viwanja vya ndege juu ya umuhimu wa kuwa na hati miliki
ya eneo hilo.
Mchumi Mkuu kutoka Tume ya Mipango, Bibi
Salome Kingdom akiongea jambo na Bw. Daniel Werema kutoka Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, wengine ni Mhandisi Omary Othman (aliyevaa t-shirt) na
Bw. Hekima Chengula kutoka Tume ya Mipango.
.................................................................................................................
Na
Adili Mhina, Mtwara.
Katika
kutekeleza Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Mamlaka ya viwanja vya Ndege
imedhamiria kufanya maboresho katika Kiwanja cha Ndege Mtwara kwa kiwango cha
Kimataifa ili kuendelea kuimarisha huduma za usafiri wa anga nchini.
Mapango
huo umeelezwa hivi karibuni na Meneja wa Teknolojia na Mawasiliano kutoka
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini , Bw. Abdulatif Min-Hajj wakati akitoa taarifa ya maendeleo
ya Kiwanja hicho kwa Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya Mipango, Bibi Florence
Mwanri alipofanya ziara katika kiwanja hicho ikiwa ni mfululizo wa ziara ya ukaguzi
wa miradi ya maendeleo unaofanywa na timu kutoka Tume ya Mipango.
Meneja
huyo alieleza kuwa mradi huo amabao ni mpango wa muda mrefu unaolenga katika kufanya
upanuzi wa kiwanja pamoja na ujenzi wa jengo la kisasa kwa ajili ya abiria upo
katika hatua za awali ambapo mkandarasi mshauri tayari amewasilisha rasimu ya
taarifa ya mpango mkuu (maste plan).
“Katika
mradi huu kiwanja cha Mtwara kitapanualiwa na kufikia code 4E ambapo kitakuwa
na uwezo wa kuhudumia ndege kama A340-200. Katika ujenzi wa jengo la abiria,
kwa awamu ya kwanza tutajenga jengo lenye mita za mraba 6570 ili kufikia
mahitaji ya mwaka 2023 na awamu ya pili tunatarajia kuwa na jengo la mita za
mraba 10,880 ili kukidhi mahitaji ya abiria kwa mwaka 2033”, alieleza Meneja
huyo.
Kwa
upande wake Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Florence Mwanri alieleza
kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo inasisitiza kuwa na vianzio mbalimbali vya
uchumi na kuwepo kwa miundombinu ya kutosha kuiwezesha Tanzania kuingia katika
nchi za kipato cha kati. Hivyo, mradi huo utasaidia kuimarisha uchumi wa nchi
sambamba na kuongeza ufanisi katika usafiri wa anga.
Aliongeza
kuwa upanuzi wa kiwanja hicho
utakapokamilika sio kwamba tu utasaidia usafiri wa anga peke yake bali kwa
upande mwingine utafungua fursa mbalimbali za uwekezaji kwa sekta binafsi na kusaidia kuongeza uchumi kwa watanzania.
“Nimeelezwa
kuwa mradi huo ukikamilika kutajitokeza fursa za uwekezaji kama kujenga
mahoteli makubwa ya hadhi ya nyota tano,
kujenga eneo la biashara, ujenzi wa
maduka na migahawa ya kisasa, ujenzi wa visima vya mafuta ya ndege,
kutakuwa na jengo kubwa la kuhifadhia mizigo, na majengo ya kutengenezea ndege.
Hizi zote ni fursa zitakazosaidia kuinua uchumi wa wananchi wetu,” alieleza.
Hata
hivyo Mwanri alishauri kuwa pamoja na kuwa na malengo mazuri ya muda mrefu mamlaka
ya hiyo inapaswa kuendelea kutekeleza
malengo yake ya muda mfupi katika kutatua changamoto za miundombinu ya barabara
za ndege kiwanjani hapo ili kuendelea kuimarisha huduma za usafiri huku
akishauri mamlaka hiyo kufanya jitihada za haraka kupata hati miliki pamoja na
kufikiria kujenga uzio katika eneo la kiwanja hicho.
“Mnapaswa
kuendelea kutekeleza mipango ya muda mfupi wakati mnasubiri mradi mkubwa
utekelezwe. Najua katika bejeti yenu ya sasa mtaendelea kukarabati miundombinu ili
ndege ziendelee kutua na kuondoka kwa usalama. Vile vile angalieni namna ya kupata
hati miliki na kujenga uzio wa eneo lote kwa ajili ya usalama na kuwadhibiti watu
wenye tabia ya kuvamia maeneo”, Alieleza Mwanri.





0 Comments