Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi
wa serikali na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro uliopo kwenye
ukumbi wa halmashauri hiyo iliyopo Wasso Desemba 15, 2016. Kushoto ni
Mkuu wa
Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya watumishi wa serikali
na halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro wakimsikiliza Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo uliopo Wasso wilayani
Ngorongoro Desemba 15, 2016.
......................................................................................................................
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Serikali itazifutia usajili Taasisi zote zisizokuwa za
Kiserikali (NGO’s) zilizoko kwenye Tarafa ya Loliondo zinazofanyakazi kinyume
na katiba zake na sheria ya nchi ambapo ametoa miezi sita zijitathimini kama zinafanya
kazi ya kuhudumia jamii au la.
Pia ameahidi
kumpeleka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Taraha
hiyo ya Loliondo kwa lengo la kuzifanyia ukaguzi NGO hizo ili kubaini kiasi cha
fedha wanazopata kama zinalingana na matokeo ya kazi za kijamii inazofanya
katika Tarafa hiyo.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Desemba 15, 2016) wakati
akizungumza na Wakurugenzi wa NGO na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Ngorongoro kwenye
ukumbi wa Halmashauri hiyo akiwa
katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.
Amesema NGO
nyingi zimekuwa zikipata bajeti kubwa ya fedha lakini masuala ya maendeleo
wanayoyafanya katika eneo hilo hayalingani na bajeti halisi wanazopata.”Loliondo
pekee kuna NGO zaidi ya 30 ila zilizokuwa ‘active’ ni 15 tu kuna nini Loliondo?
Na baadhi yake zinafanya kazi ya kuchochea eneo hili lisiwe na amani,”.
Waziri Mkuu
ameongeza kuwa “watu wote wanaoshirikiana na NGO hizo zinazochafua taswira ya
nchi tutawashughulikia. Mnawavalisha watoto kandambili zilizotobona na miguu
michafu kisha mnawapiga picha mnazituma kwenye mitandao na kusema umasikini wa
Tanzania ndio huo. Hatutawavumilia watu wa namna hii,” amesisitiza.
Amesema NGO
nyingi zimekuwa zikilalamikiwa kutokana na kufanya kazi kinyume na mikataba
yake ya usajili na miongoni mwa NGO hizo ni pamoja na PWC inayopata sh. bilioni
2.5 kwa mwaka, UCRT inayopata sh. bilioni 1.5 kwa mwaka, Oxfarm Tanzania inayopata
sh. bilioni 1.7 kwa mwaka.
“Nitafuatilia
kwa karibu kuona kazi wanazozifanya kwani zinapata fedha nyingi kwa mwaka. Lazima
tujenge nidhamu kwa wote wanaopata fedha kwa lengo la kuisaidia jamii. Wote
wanaojihusisha na shughuli nje ya mikataba yao wabadilike ndani ya miezi sita.
Wafuate kanuni, sheria na taratibu za nchi,” amesema.
Amesema
Serikali haiwezi kufanya kazi bila ya wadau ila haiitaji wadau wanaofanya mambo
kinyume cha taratibu, ambapo amezitaka NGO hizo kusajiliwa na Wakala wa Usajili
wa Kampuni (BRELA) ili ziweze kutambulika kisheria na ofisi zake kujulikana
badala ya hivi sasa kuwa na ofisi za mifukoni.
Awali, Waziri
Mkuu alizungumzia na wananchi wa kijiji cha Ololosokwan ambapo alisema mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa Tarafa la
Loliondo na wawekezaji unaolikabili eneo hilo Waziri Mkuu mesema Serikali itahakikisha
mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu unamalizika haraka.
Aidha, amemwagiza
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo kukutana na uongozi wa wilaya ya
Ngorongoro na kamati ya wananchi iliyoundwa kwa ajili ya kuboresha uhifadhi ili
kumaliza mgogoro huo na kisha kumpelekea taarifa.
“Haiwezekani
Waziri Mkuu aje kumaliza mgogoro wa ardhi Loliondo wakati kuna viongozi hapa.
Mimi nimemuagiza Mkuu wa mkoa aje akutane na wawekezaji na wananchi ili
kuzungumza na kuupatia ufumbuzi mgogoro huu na atakayeshindwa ndiye
nitakayemshughulikia,” amesema.
Amesema
Serikali itahakikisha migogoro ya ardhi inamalizika nchini ili kuwawezesha
wananchi kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu. “Naomba tushirikiane katika
kutatua changamoto hii ya migogoro ya ardhi kwani suala hili limeahidiwa katika
ilani ya uchaguzi ya CCM,”.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amepiga marufuku tabia
ya baadhi ya wananchi kuingiza ng’ombe kiholela kutoka nje ya nchi kwa kuwa
kitendo hicho kinachangia kuwepo kwa migogoro ya ardhi.
Katika
kuhakikisha suala hilo linadhibitiwa Waziri Mkuu amemtaka Mkuu wa wilaya hiyo,
Bw. Rashid Taka kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo
kuimarisha ulinzi katika mipaka kwa kuongeza doria ili kudhibiti uingiaji
holela wa mifugo.
Naye
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema eneo la Loliondo ni muhimu sana kwa ajili ya
ikolojia ya wanyama pamoja na maji kwani hifadhi ya Serengeti inategemea zaidi
eneo hilo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, DESEMBA 15, 2016.


0 Comments