Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Kassim Majaliwa akitoa hotuba fupi kwa Maafisa na askari wa Jeshi la
Magereza alipofanya ziara ya kikazi ya
kukagua maandalizi ya ujenzi wa nyumba 320 za makazi ya askari katika eneo la
Gereza Kuu Ukonga, Jiji la Dar es Salaam Disemba 24, 2016.
........................................................................................................................................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea gereza la Ukonga jijini Dar es
Salaam na kukagua eneo la ujenzi wa makazi ya askari wa Magereza unaotarajiwa
kuanza baada ya wiki tatu zijazo.
Akizungumza na askari wa magereza kabla ya kufanya ukaguzi huo leo (Jumamosi,
Desemba 24, 2016) Waziri Mkuu amesema ziara aliyoifanya leo, ni ufuatiliaji wa
maagizo ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli aliyoitoa wakati alipoenda kukagua
gereza hilo.
Novemba 29, mwaka huu, Rais Magufuli alifanya ziara kwenye gereza hilo
na kupokea taarifa ya uhaba wa nyumba za kuishi askari wa jeshi hilo zipatazo
9,500 na akaagiza zitafutwe sh. bilioni 10 haraka ili kupunguza tatizo hilo.
Akizungumzia kuhusu ujenzi huo, Waziri Mkuu amesema amefarijika kukuta Wakala
wa Majengo Tanzania (TBA) wako eneo la kazi na wameanza kusafisha eneo hilo.
“Nimefarijika kukuta TBA wako kazini na nimeelezwa hatua inayofuata ni
upimaji wa sampuli za udongo kabla hawajaanza kujenga msingi. Nawapongeza TBA
kwa kazi nzuri wanazofanya za ujenzi wa nyumba zenye viwango na kwa haraka kama
tulivyoona kule Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na nyumba za Magomeni Kota,”
amesema.
Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua mchango uliofanywa na Serikali ya
awamu ya nne katika suala la makazi ya askari kama vile wa Jeshi la Wananchi (JWTZ)
na Jeshi la Polisi. “Nia ya Serikali ni kuhakikisha makamanda wote wanapata nyumba
nzuri ili waendelee kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa wakiwa na uhakika
familia zao zimetulia kwenye makazi bora”.
Amesema katika ziara alizozifanya kwenye mikoa mbalimbali, alitembelea
magereza ya Isanga, Msalato (Dodoma), Lindi, Singida na Keko (Dar es Salaam) alikuta
nyumba za askari hazina viwango na kama zipo zimechakaa sana.
Mapema,
akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa nyumba hizo, Kaimu Kamishna Jenerali wa
Magereza, Juma Malewa alisema wanamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwapatia fedha
za ujenzi wa makazi ya askari na kwamba jeshi hilo litafanya kazi zote zisizo za
kitaalamu ili kuokoa fedha za Serikali na badala ya kulipwa watu binafsi, fedha
hizo zitatumika kuongeza nyumba zaidi.
“Tumekubaliana na TBA kazi zote zisizohitaji utalaamu kama kufyatua
matofali, kubeba mizigo au kufyeka zitafanywa na askari wetu pamoja na wafungwa
ili tuokoe gharama zote hizo na badala ya kulipa watu binafsi, fedha hizo zitumike
kujenga nyumba nyingine 80,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema wamejipanga kufanya kazi hizo kwa saa 24 kila siku ili kuokoa
muda ambao TBA walikuwa wameuweka wa kukamilisha ujenzi ndani ya miezi minane.
Alisema wako tayari kuanzisha kambi za ujenzi kwa kutumia wafungwa na
askari ili wafanye kazi zisizohitaji utaalamu na fedha zitakazopatikana, badala
ya kuwalipa watu binafsi zitumike kujenga nyumba zaidi za askari.
Naye
mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TBA, Bw. Baltazar Kimangano alisema wanataraji
kuanza ujenzi ndani ya wiki tatu baada ya kupokea matokeo ya uchunguzi wa
sampuli za udongo kutoka taasisi ya BICO ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alisema wanataraji kujenga majengo (block) manne ya ghorofa sita kila
moja ambayo kwa ujumla yatakuwa na nyumba 240 zenye ukubwa wa vyumba viwili vya
kulala. Pia watajenga majengo (block) mengine mawili ya ghorofa sita kila moja ambayo
yatakuwa na nyumba 80 zenye ukubwa wa vyumba vitatu vya kulala.


0 Comments