*Aagiza arudishwe Longido kujibu tuhuma zinazomkabili
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza na watumishi wa serikali na Halmashauri ya Wilaya
ya Ngorongoro uliopo kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo
iliyopo Wasso Desemba 15, 2016. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha,
Mrisho Gambo.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
.................................................................................................................
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi aliyekuwa Mwekahazina wa Halmashauri ya
Wilaya ya Longido, Bw. Issai Mbilu ambaye kwa sasa amehamishiwa Wilaya ya Bahi
mkoani Dodoma na kuagiza arudishwe haraka na kuja kujibu tuhuma za ubadhilifu sh.
milioni 642.4 za miradi zinazomkabili.
“Tunaendelea
kudhibiti na kuweka nidhamu ndani ya Serikali. Ukiharibu Longido usitegemee
kuhamishiwa wilaya nyingine tunamalizana hapa hapa. Hatuwezi kuhamisha ugonjwa
hapa na kuupeleka wilaya nyingine hivyo Mwekahazina huyu arudishwe haraka
Longido,” amesisitiza.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Desemba 16, 2016) wakati akizungumza na
watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo
akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.
Pia
amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Bw. Richard Kwitega kumuandikia
barua Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) akimuomba amrudishe Mwekahazina huyo katika kituo chake cha kazi cha
zamani ili aweze kujibu tuhuma zinazomkabili.
Amesema
Serikali haitamvumilia mtumishi wa idara yoyote atakayeharibu jambo halafu
kuhamishwa sehemu nyingine, “hivyo naagiza kuanzia sasa nimemsimamisha kazi Mwekahazina
huyu na arudi hapa kujibu kwanini ameleta hasara ya hizi fedha. Na nyie
watumishi wengine hili liwe funzo kwenu,” amesema.
Amesema
miradi mingi ya maendeleo inakwama kwa sababu ya baadhi ya watumishi kuweka
mbele maslahi binafsi badala ya kuzingatia maadili ya utumishi, hivyo amewaagiza
Wakuu wa Idara wafuatilie kwa makini miradi
inayotekelezwa katika maeneo yao kama inalingana na thamani halisi ya fedha
zilizotolewa.
Akizungumzia
kuhusu kushamiri kwa biashara haramu ya dawa za kulevya wilayani Longido,
Waziri Mkuu amewaagiza wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya kufanya
kufanya msako wa nyumba hadi nyumba na kuwakamata wote watakaokutwa wanafanya
biashara hiyo.
“Wilaya
hii ina sifa mbaya ya kuwa kitovu cha kusafirisha dawa ya kulevya zikiwemo bangi na mirungi. Hivyo nawaagiza wajumbe wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama waendeshe msako kwa kila nyumba na atakayekamatwa
achukuliwe hatua. Dawa za kulevya zinadhohofisha nguvu kazi ya Taifa,”.
“Ukivuta
bangi unapishana na kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu kwani unakwenda kulala jambo
ambalo hatuwezi kulikubali. Watakaokutwa wanauza au kununua mirungi na bangi
wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa pamoja na kutaifisha magari
yanayotumika kubeba bidhaa hiyo haramu,” amesema.
Awali,
Mkuu wa Wilaya hiyo Bw. Daniel Chongolo akisoma Taarifa ya Wilaya amesema
Longido inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutumika kama njia kuu ya
kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi kwenda nchi jirani ya
Kenya ambako biashara hiyo imehalalishwa.
Changamoto
nyingine ni ukosefu wa hospitali ya wilaya hali inayofanya wananchi kwenda
kutibiwa Kenya, ambapo Waziri Mkuu alisema haiwezekani wakakosa hospitali ya
wilaya hivyo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikiusha anatenga
fedha za ujenzi huo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali ipo
mbioni kujenga kiwanda cha kuchakata madini ya magadi soda ili yawe na ubora na
thamani kubwa. Ametoa kauli hiyo aliposimamishwa
na wananchi katika kijiji cha Loonolwo kilichopo Kata ya Gelai Merugoi Wilayani
Longido akitokea wilayani Ngorongoro.
Amesema
lengo la kujenga kiwanda hicho ni kuwawezesha wananchi wa wilaya hiyo hasa
akinamama wanaoishi karibu na Ziwa Natron linalotoa magadi hayo waweze
kunufaika na uwepo wa ziwa hilo.
Waziri
Mkuu amesema ujenzi wa kiwanda hicho utawezesha vijana na akinamama hao
wanaouza magadi maeneo ya pembezoni mwa barabara katika ziwa Natron kupata
ajira kwa kuwa kitazalisha ajira zaidi ya 500 katika wilaya hizo mbili za
Longido na Ngorongoro.
Pia
amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo kushirikiana na wataalam
wake kufanya tathimini ya uhaba wa chakula katika wilaya za Longido na
Ngorongoro ili Serikali ijue Mkoa wa Arusha una ukosefu wa chakula kwa kiasi
gani.
"Gambo
fanya tathimini ya hali ya njaa katika wilaya hizi mbili ili tuweze kuwasaidia
wananchi hawa. Hata hivyo nawaomba wananchi mtunze kiasi cha chakula
mlichonacho na marufuku tumia nafaka kwa ajili ya kupika pombe,” amesema.
Awali,
wananchi hao waliokuwa na mabango mbalimbali walilalamikia kero ya mipaka ya
ardhi kati ya vijiji vya wilaya za Longido na Ngorongoro, ambapo Waziri Mkuu
alimuagiza Afisa Ardhi Mkoa wa Arusha, Bw. Hamdoun Mansour kwenda katika vijiji
hivyo vya mpakani na kukutana na viongozi wa kimila ili kumaliza mgogoro huo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, DESEMBA 16, 2016.

0 Comments