Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja
wa Mabewani mjini Makete, januari 20, 2017.
(Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
...........................................................................
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema katika mwaka huu wa fedha Serikali imetenga sh.
bilioni 19 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Njombe-Makete yenye urefu wa
kilomita 109.4 kwa kiwango cha lami.
Ametoa
kauli hiyo jana (Ijumaa, Januari 20, 2017) wakati akizungumza na viongozi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Makete alipowasili katika kata ya Mtamba wilayani hapa
akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Njombe.
Waziri
Mkuu amesema usanifu wa kina wa barabara ya Njombe-Makete kwa ujenzi wa kiwango
cha lami umekamilika hivyo amewataka wananchi waendelee kuwa na subira.
Amesema
barabara nyingine inayotarajiwa kujengwa ni ya kutoka Makete hadi Mbeya kupitia
Isyonji yenye urefu wa kilomita 96 ambayo imetengewa sh. milioni 50 kwa ajili
ya kufanyiwa usanifu.
Waziri
Mkuu amesema wananchi waendelee kushirikiana na Serikali kwani imedhamiria
kuwatumikia kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maeneo yao.
Aidha,
Waziri Mkuu amewataka wahandisi wa wilaya hiyo kuhakikisha wanawasimamia vizuri
wakandarasi wanaojenga miradi mbalimbali katika halmashauri zao kuhakikisha
kama viwango vinalingana na thamani halisi ya fedha zinazotolewa.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka wakuu wa Idara katika halmashauri
kupambana na vitendo vya rushwa na wahakikishe watumishi hawatowi huduma kwa
kuomba rushwa.
“Kwanza
watumishi watambue kwamba rushwa ni dhambi. Pia kiutumishi ni makosa makubwa
hivyo wajiepushe na vitemdo hivyo,” amesema.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Makete Bi. Veronica Kessy amesema kujengwa kwa barabara
hizo kwa kiwango cha lami kutaimarisha ukuaji wa uchumi wa wilaya hiyo na Mkoa
wa Njombe kiujumla hivyo wananchi kupata tija.
“Mfano
barabara ya kutoka Makete hadi Mbeya kupitia Bulongwa, Iniho, Kikondo na
Isyonje itasaidia wilaya kufunguka hivyo kurahisisha usafirishaji wa mazao ya
misitu kama mbao,” amesema.
Hata
hivyo Mkuu huyo wa Wilaya amesema barabara hii pia itaunganisha Wilaya hiyo na
kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Songwe hivyo watapata fursa ya kuanzisha
kilimo cha maua. Awali walishindwa kulima maua kwa sababu hakukuwa na usafiri
wa uhakika.
Awali
Waziri Mkuu alitembelea shamba la mifugo la Kitulo linalomilikiwa na Wizara ya
Kilimo, Mifugo na Uvuvi lenye jumla ya Ng’ombe 750 wakiwemo ndama 61, majike
212, mitamba 273, madume 21, na madume wadogo 183.
Shamba
hilo linazalisha wastani wa lita 450,000 za maziwa kwa mwaka kutokana na
ng’ombe 123 wanaokamuliwa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, JANUARI 21, 2017.

0 Comments