Mkuu wa Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu.
.................................................
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Imebainika kwamba idadi ya wanaume wanaotoa malalamiko yao dhidi ya wenza wao imeongezeka karibu mara mbili kwa mwaka 2016 ikilinganishwa na mwaka juzi 2015.
Akitoa taarifa hiyo ofisini kwake Mkuu wa Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu alisema kwamba idadi hiyo imeongezeka kutoka walalamikaji 34 mwaka 2015 hadi kufikia 63 mwaka 2016 ambapo ni sawa na 48%.
Alisema ongezeko hilo limetokana na kuenea kwa elimu inayotolewa na askari wa kitengo cha Dawati kwa watu wa jinsia zote kupitia vyombo vya habari hasa radio zilizopo jijini hapa. Alisema mbali na radio pia dawati hilo limetoa elimu kupitia vikao vya wazazi katika shule ya Msingi Osunyai na Shule ya Msingi Burka zilizopo halmashauri ya jiji la Arusha ambayo imewasaidia wananchi kujua haki zao na wapi waanzie pindi wanaponyanyaswa ndani ya ndoa zao.
Mkuu huyo wa kitengo cha Dawati la Jinsia na watoto mkoa wa Arusha alisema wengi wa wanaume hao huwa wanafanyiwa ukatili wa Kisaikolojia ambapo baadhi ya wenza wao wanaonekana kutowathamini lakini wengine kukataa kushiriki tendo la ndoa.
“Mbali na Ukatili wa Kisaikolojia pia baadhi yao wanafanyiwa Ukatili wa kiuchumi ambapo baadhi ya wanawake wenye uwezo kuwazidi waume zao huwa wakati mwingine wanatoa maamuzi ya kifamilia pengine yakawa na maendeleo lakini bila kuwashirikisha wenzi wao hali ambayo inawafanya wenzao wabaini kwamba hali hiyo inatokana na kuzidiwa kipato na hivyo kushindwa kutengua maamuzi au kutoa ushauri”. Alisema Mkuu huyo wa Dawati.
Mkuu huyo wa Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha alitaja wilaya inayoongoza kwa idadi ya wanaume kuripoti malalamiko yao katika ofisi yake ni Arusha ambayo ilikuwa na jumla ya walalamikaji 48, Arumeru 8, huku Ngorongoro ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na walalamikaji watatu. Wilaya ya Longido ni ya nne ambayo ilikuwa na walalamikaji wawili huku Karatu na Monduli zilikuwa zina mlalamikaji mmoja kila wilaya.
Mkuu huyo wa Dawati alitoa wito kwa viongozi wa kata, mitaa, vijiji na hata vitongoji kuiarifu ofisi yake pindi wanapokuwa na vikao katika maeneo yao ili waweze kuzidi kusambaza elimu ya ukatili wa kijinsia kwa wanandoa kupitia vikao hivyo kwani wanaume wengi awali walikuwa hawana ufahamu kama wao pia wanaweza kutoa malalamiko yao kupitia dawati hilo.
Ofisi ya Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha mwishoni mwa mwaka jana imekuwa ikitoa elimu ya ukatili wa jinsia kwa wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi zilizopo katika halmashauri ya jiji la Arusha ambazo ni Sombetini, Osunyai,Ngarenaro, Kaloleni, Burka na Elerai hali ambayo imewasaidia wanafunzi hao kupata uelewa mkubwa juu ya ukatili.......................................

0 Comments