![]() |
| Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na
waumini wa Kanisa Kuu la Jimbo katoliki Bukoba mkoani Kagera mara baada ya
Ibada. PICHA NA IKULU |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amewahakikishia Watanzania kuwa licha ya Mamlaka ya udhibiti wa huduma za
Nishati, Maji na Mafuta (EWURA) kuridhia ombi la TANESCO la kupandisha bei ya
umeme kuanzia Januari mosi,2017 bei ya umeme haitapanda.
Rais Dkt. Magufuli amezungumza hayo leo Jumapili ya Januari Mosi, 2016
wakati wa Ibada katika Kanisa la Bikira Maria Mama Mwenye Huruma,Kanisa
Kuu Jimbo Katoliki la Bukoba anapoanza rasmi ziara ya kikazi ya siku mbili
Mkoani Kagera.
Rais Magufuli ameshangazwa na kitendo cha watendaji waliopandisha bei ya
umeme bila hata ya kushauriana na yeye, Makamu wa Rais,Waziri Mkuu au Waziri
mwenye dhamana ya Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo na hivyo kumshukuru
Waziri Muhongo kwa kutengua maamuzi hayo.
''Ninamshukuru sana Waziri wa Nishati na Madini kwa maamuzi ya kusitisha
hayo kwa hiyo umeme hakuna kupanda bei,haiwezekani unapanga mikakati ya kujenga
viwanda na hasa katika mikakati mikubwa ya nchi ya kusambaza umeme mpaka
vijijini,na umeme huu unaenda kwa watu masikini walioumbwa kwa mfano wa Mungu
halafu mtu pekee kwa sababu ya cheo chake anapandisha bei,hili haliwezekani''
Alisema Rais Dkt. Magufuli.''
Aidha, Rais Dkt Magufuli ameendelea kuwataka watanzania katika mwaka huu
mpya 2017 kuendelea kufanya kazi kwa bidii kama maandiko matakatifu
yanavyoelekeza kuwa asiyefanya kazi na asile badala ya kulalamika kuwa fedha
zimepotea.
Kwa upande wake,Askofu Msaidizi Jimbo Katoliki la Bukoba,Askofu
Methodius Kilaini,akitoa mahubiri kwa waumini waliohudhuria ibada hiyo
amempongeza Rais Dkt Magufuli kwa uongozi wake imara,huku akisema kupungua kwa
urasimu katika ofisi za umma kunatokana na utendaji kuongezeka na
kuwataka wana Kagera na Watanzania kwa ujumla kumuunga mkono Rais Magufuli kwa
kufanya kazi kwa bidii na uaminifu.
Mara baada ya Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo
Katoliki la Bukoba,Askofu Desderius Rwoma,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt John Pombe Magufuli aliwatakia heri ya mwaka mpya waumini wa
kanisa hilo na watanzania kwa ujumla.
Jaffar
Haniu
Naibu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kagera.
01
Januari, 2017

0 Comments