*Ni wale waliohusika na upotevu wa sh. milioni 700
Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wa kijiji cha Lusitu wilayani Ludewa
walioziba barabara wakitaka asimame na
kuwasalimia alipokuwa akitoka kwenye mgodi wa chuma wa Liganga kwenda mjini
Ludewa Januari 26, 2017.
(Picha na Ofisi
ya Waziri Mkuu)
Wananchi wa kijiji cha Lusitu wilayani
Ludewa wakilizuia gari la Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa wakimtaka asimame
na kuwasalimia alipokuwa akienda mjini Ludewa kutoka mgodi wa chuma wa Liganga
Januari 26, 2017. Mheshimiwa majliwa alisimama na kuwahutubia.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi
wa dini baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Halmashauri, mjini
Ludewa Januari 26, 2017.
....................................................................................................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe Bw.
Christopher Ole Sendeka kuwachukulia hatua watumishi Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa waliohusika na
upotevu wa fedha za maendeleo.
Amesema zaidi
ya sh. milioni 700 zilizopelekwa katika halmashauri kwa ajili ya miradi mbalimbali
ya maendeleo zikiwemo sh. milioni 300 za ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri hiyo.
Waziri Mkuu ametoa
kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Januari 26, 2017) wakati akizungumza na
wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Halmashauri alipokuwa
katika ziara yake katika Wilaya ya
Ludewa mkoani Njombe.
“Mkuu wa Mkoa
watu wote waliohusika na upotevu huu watafutwe popote walipo na kuchukuliwa
hatua na kisha nipewe taarifa ya hatua ulizochukua. Hatuwezi kuwavumilia watu hao
ambao wanachora ramani kwa sh milioni 200
na sh. milioni 100 zingine hazijulkikani zilipo,“ alisema.
Pia
Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu huyo wa Mkoa
kufuatilia kiasi kingine cha sh milioni 400 zilizopelekwa wilayani hapo
kwa ajili ya maendeleo ambazo nazo hazijulikani zilipo. “Tafuta waliohusika
popote walipo hata kama ni nje ya Njombe waje kutueleza ziliko fedha zetu,”
Mbali
na kutoa agizo hilo kwa Mkuu wa Mkoa, pia Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa
Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini (TAKUKURU) kuhakikisha
inashirikiana nayo inafanya uchunguzi ili kubaini watu waliohusika na upotevu
huo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema
Serikali haitowavumilia watumishi wote wanaojihusisha na vitendo vya ubadhilifu
wa fedha za umma, hivyo amewataka watumishi wafanye kazi kwa kuzingatia sheria
na maadili.
Waziri
Mkuu aliwataka watumishi wa umma nchini kuacha tabia ya kudokoa fedha za
maendeleo zinazopelekwa katika Halmashauri zao kwa sababu Serikali iko macho na
itawashughulikia wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Aidha,
Waziri Mkuu alitoa wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kusimamia
vizuri fedha za maendeleo zinazopelekwa kwenye maeneo yao na kuhakikisha
zinatumika kama ilivyokusudiwa.
Awali
akiwa njiani kuelekea Ludewa Mjini akitokea katika kata ya Mundindi Waziri Mkuu
alisimamishwa na wananchi wa kijiji cha Mlangali ambao waliiomba Serikali
iwasaidie kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo ya
maji.
Mwenyekiti
wa kijiji hicho Bw. Michael Lameck alisema alimueleza Waziri Mkuu kwamba awali
walikuwa wanapata maji ila kwa sasa hayatoki kutokana na uchakavu wa
miundombinu hali iliyowafanya kuchangishana na kupata sh. milioni 95 kati ya
200 zinazohitajika.
Kufuatia
hali hiyo Waziri Mkuu alimuagiza
Mhandisi wa Maji wa Wilaya hiyo, Bw. Nasib Mlenge kwenda kijijini hapo leo Januari 27 kukutana na Bw. Lameck ili
kushirikiana naye na kuangalia alipofikia na kuendeleza uboreshaji wa
miundombinu hiyo ili wananchi hao wapate maji.
“Mwenyekiti
amechangisha sh. milioni 95 na kununua baadhi ya vifaa nyinyi mnashindwa nini.
Lazima muwe makini na matatizo ya wananchi na Serikali haitaki masuala ya
urasimu. Watu wana shida ya maji na mnajua tatizo mmekaa tu,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, JANUARI 27, 2017.



0 Comments