WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza viongozi wa Idara ya Uhamiaji kuandaa semina za
mafunzo ya elimu ya uraia kwa wahudumu ya hoteli na nyumba za kulala wageni
nchini ili kudhibiti wimbi la wahamiaji haramu.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Alhamisi,
Januari 19, 2017) mara baada ya kuwasili katika Ikulu ndogo ya Njombe na
kupokea taarifa ya mkoa wa Njombe iliyotolewa na mkuu wa mkoa huo Bw. Christopher
Ole Sendeka.
Katika taarifa hiyo Bw. Ole Sendeka
alisema kwenye kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba, 2016 Idara ya Uhamiaji
ilibaini kuwepo kwa raia 119 wa kigeni ndani ya mkoa huo, ambapo wahamiaji
haramu 42 walikamatwa.
Waziri Mkuu alisema ni hatari kwa mkoa
huo kuwa na idadi kubwa ya raia wa kigeni walioingia nchini bila ya kufuata
utaratibu hivyo aliitaka Idara hiyo ijipange vizuri ili kudhibiti watu wa aina
hiyo.
“Anzisheni utaratibu wa kutoa semina
kwa wahudumu wa hoteli na nyumba za kulala wageni. Hawa wakipata elimu ya uraia
watawasaidia katika kutoa taarifa za kuwepo kwa wageni ambao wana mashaka na uraia
wao,” alisema.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa mikoa kujikita katika ukusanyaji wa mapato
pamoja na kuzuia mianya ya rushwa pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma
katika maeneo yao.
Alisema lazima kuwe na nidhamu ya
matumizi ya fedha za Serikali zinazopelekwa katika halmashauri nchini. “fedha
hizo lazima zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa yenye kuleta tija kwa wananchi
na Taifa kwa ujumla,”.
Aidha, Waziri Mkuu aliwataka
watumishi wa umma kuibua maeneo mapya ya ukusanyaji wa mapato ambayo yatatumika
katika utoaji wa huduma za jamii hivyo kuleta tija kwa Taifa.
Pia aliwataka wakuu wa mikoa na
wilaya kusimamia vizuri miradi ya maendeleo inayojengwa katika maeneo yao
kuhakikisha kama inalingana na thamani halisi ya fedha zinazotolewa na wasikubali
kupokea miradi iliyojengwa chini ya kiwango.
Awali Mkuu wa mkoa huo alisema kati
ya wahamiaji haramu 42 waliokamatwa 39 ni raia wa Ethiopia, wengine wanatoka
Uganda (1), Burundi (1) na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (1). Wote
walifikishwa mahakamani na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Alisema Idara ya Uhamiaji
inaendelea na mikakati ya kuishirikisha
jamii katika utoaji wa taarifa pindi wanapowatilia shaka kuhusu ukaazi wao
ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya uraia na upanuzi wa huduma za uhamiaji.
Akizungumzia kuhusu suala la
ukusanyaji wa mapato mkuu wa mkoa alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha
2015/2016 mkoa uliweza kukusanya kiasi cha sh. bilioni 7.07 sawa na asilimia
89.3 ya makisio ambayo yalikuwa sh. bilioni 7.92.
“Kwa kipindi cha mwaka wa fedha
2016/2017 halmashauri zilikisia kukusanya kiasi cha sh. bilioni 8.22 ambapo
katika kipindi cha nusu mwaka (Julai hadi Desemba, 2016) wameweza kukusanya
jumla ya sh. bilioni 4.37 sawa na asilimia 53.2 ya makisio ya mwaka,” alisema.
Alisema mafanikio hayo yamechangiwa
na ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mashine maalumu za kielektroniki za
kukusanyia mapato pamoja na kuondoa utaratibu wa ukusanyaji wa mapato kwa kutumia
mawakala katika vyanzo vingi.
Aidha, Ole Sendeka alisema
halmashauri za mkoa huo zinaendelea kupitia upya sheria ndogo za ukusanyaji wa
mapato ili kuongeza vyanzo vya mapato pamoja na baadhi ya viwango vya kodi na
tozo mbalimbali.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, JANUARI 20, 2017.
0 Comments