Meneja Mifumo ya Kielektroniki
ya Forodha kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Tinkasimile Felix (kushoto) akipokea tuzo ya ubunifu wa
mfumo wa TANCIS kutoka
kwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Mindi Kasiga.
Mfumo
huu wa TANCIA umeundwa kwa kuzingatia kanuni za hali ya juu za
kiteknolojia kwa lengo la kuongeza ufanisi, uharaka, uwazi na uhakika
katika usimamizi wa masuala ya forodha.
................................................................................
Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) imepata tuzo kutoka Umoja wa Afrika
(AU) kutokana na mfumo wa Uondoaji Mizigo Bandarini (TANCIS) ambao unafanya
kazi kwa ufanisi na uharaka zaidi pamoja na kudhibiti mianya ya rushwa.
Tuzo hiyo imetolewa na Umoja wa Nchi za Afrika
jijini Addis Ababa Ethiopia, baada
ya kufanyika shindano la Taasisi za Serikali za Umoja wa Nchi hizo kutokana na kuboresha mifumo ya utendaji
kazi katika taasisi zao.
Akizungumza
kwa niaba ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi.
Mindi Kisiga amesema kuwa TRA na Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii (SSRA) ndiyo taasisi pekee za Serikali zilizoweza kufanya vizuri katika
ubunifu katika utendaji wa taasisi hizo.
“Tuzo hizi
zinatolewa na nchi za Umoja wa Afrika kwa taasisi za Serikali ambapo
hushindanishwa katika masuala ya ubunifu katika utendaji kazi wa taasisi husika,”
alisema Bi. Mindi.
Akizungumza
kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Alphayo Kidata, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi
toka Mamlaka ya Mapato Tanzania Bw. Richard Kayombo alisema TRA imeshinda tuzo
hiyo kutokana na ubunifu wa mfumo wa TANCIS ambao umeundwa kwa kuzingatia
kanuni za hali ya juu za kiteknolojia kwa lengo la kuongeza ufanisi, uharaka,
uwazi na uhakika katika usimamizi wa masuala ya forodha.
Alisema mfumo
huu umeunganishwa na mifumo mingine ya TRA na ya wadau muhimu ambao wanahusika
katika uondoshaji wa bidhaa katika udhibiti wa forodha .
“Mfumo wa
TANCIS humwezesha mwagizaji wa bidhaa kufuatilia hatua iliyofikiwa katika kuondosha bidhaa zake kwa kutumia simu
ya kiganjani au kifaa kingine chochote cha kielektroniki hivyo mfumo huu
unarahisisha utoaji huduma na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato,” alisema
Bw. Kayombo.
Kwa upande
wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano toka Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii (SSRA) Bi. Sarah Kibonde
alisema kuwa taasisi yake imepokea tuzo hiyo ya ubunifu kwa
kupitia mfumo wa kanzidata ya Taifa ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii.
Alisema TRA iliwawezesha kupata taarifa zilizohusu walipajikodi wa (PAYE)
ambazo zilifanikisha uchambuzi wa waajiri wasiochangia Mifuko ya Jamii.

0 Comments