WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuhakikisha eneo la Kisarawe ii
linakuwa na umeme wa uhakika ili kuwezesha viwanda na wananchi wa eneo hilo kupata
nishati hiyo.
Alitoa agizo hilo jana jioni (Jumanne, Januari 3, 2017) wakati
alipotembelea kiwanda cha Milkcom kinachozalisha bidhaa za maziwa na kiwanda
cha Watercom kinachozalisha maji vilivyoko katika kata ya Kisarawe ii wilayani
Kigamboni akiwa katika ziara yake ya kikazi
“Waziri wa Nishati ahakikishe eneo hili linapata umeme wa uhakika
ili kuviwezesha viwanda hivi kufanyakazi vizuri jambo litakaloongeza
uzalishaji. Pia wananchi wanaoishi katika maeneo haya nao watanufaika na
upatikanaji wa nishati hiyo,” alisema.
Waziri Mkuu alisema amefarijika na jitihada
za muwekezaji huyo za kuungamkono mkakati wa Serikali ya awamu ya Tano wa
kuifanya Tanzania kujenga uchumi wa viwanda utakaoliwezesha Taifa kufikia
uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Awali, Msemaji wa Viwanda hivyo, Aboubakar
Faraj akisoma taarifa ya viwanda hivyo kwa Waziri Mkuu alisema moja ya
changamoto zinazowakabili ni pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika jambo
linasababisha kupanda kwa gharama za uzalishaji.
“Punde umeme unapokatika tunalazimika kutumia
majenereta kwa muda mrefu. Hii husababisha ongezeko la gharama za uzalishaji
ambazo huumiza kiwanda kwa sababu haiwezekani kumtwisha mzigo huu mlaji,”
alisema.
Faraji alisema changamoto nyingine ni
miundombinu ya barabara ambayo usababisha wateja wengi kushindwa kufika kwenye
viwanda hivyo kwa urahisi, hivyo aliiomba Serikali kuwatatulia kero hilo.
Aliongeza kuwa kwa sasa viwanda hivyo
vimeajiri watu zaidi ya 1,800, ambapo alisema endapo Serikali itawahakikishia
upatikanaji wa umeme na barabara wataongeza ajira kwa asilimia 25 ifikapo mwaka
2018.
Mapema Waziri Mkuu
alizindua wodi ya wazazi katika Zahanati ya Kisarawe ii iliyojengwa kwa
ufadhili wa kampuni ya mafuta ya Oilcom. Wodi hiyo yenye vyumba vitatu
itawapunguzia akinamama kusafiri umbali mrefu kutuata huduma hiyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
JUMATANO, JANUARI 4, 2017
No comments:
Post a Comment