WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa ameagiza walimu wanaishi mbali na shule wakati shule zao zina majengo
wahame mara moja na warudi kuishi kwenye nyumba za shule.
Amesema
haifai kuacha walimu waishi mbali na maeneo ya shule kwani hali hiyo inachangia
uchelewaji kazini na inapunguza muda wa kuwasimamia wanafunzi au kuwasaidia
jioni pale wanapohitajika kufanya hivyo.
Ametoa agizo
hilo wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Chingumbwa, kata ya Mbekenyera,
wilayani Ruangwa jana mchana (Ijumaa, Desemba 30, 2016) kwenye mkutano
uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi kijijini hapo.
“Nimeambiwa
kuwa walimu wako wachache kwa sababu hapa shuleni hakuna nyumba za kuishi
walimu. Mbona wanakaa Mbekenyera? Watawezaje kuwahi kazini asubuhi wakati
hawana magari? Mvua ikinyesha watafikaje shuleni? Kuanzia leo, walimu wote warudi
mara moja na waje kupanga hapa kijijini kwa sababu nyumba zipo,” amesisitiza.
“Uamuzi wa
walimu kuishi jirani na shule ulifikiwa ili mwalimu awepo na kuwasimamia
wanafunzi wakati wakifanya usafi na wakati mwingine aweze kutoa msaada kwa
wanafunzi wanaojisomea jioni pindi wakihitaji msaada au ufafanuzi,” amesema.
Pia Waziri
Mkuu amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Bw. Andrea
Chezue asimamie zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha anapunguza walimu
walioko Ruangwa mjini na kuwahamishia shule za vijijini ambako kuna upungufu wa
walimu.
Amesema ili
kusaidia juhudi za Serikali za kuboresha elimu nchini, ni vema kila kijiji
kikaweka utaratibu wa kuchangia matofali ili iwe rahisi kuanza ujenzi wa nyumba
za walimu.
Akiwa katika
kijiji cha Mkutingome, Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa
aliwahamasisha wakazi wa kijiji hicho wachangie matofali 100 kutoka kila kaya
ili yapatikane matofali 40,000 yatakayotumika kujenga zahanati ya kijiji hicho.
Yeye aliahidi
kuwachangia mabati 150 ambayo kati yake, mabati 100 yatatumika kuezekea
zahanati ya kijiji na mengine 50 yatatumika kukamilisha nyumba ya Mwalimu
ambayo imekaa kwa muda mrefu bila kumaliziwa.
Katika
kuhakikisha ujenzi wa zahanati hiyo unaanza mara moja, Mkurugenzi wa kampuni ya
ujenzi ya Wanyumbani Construction, Bw. Fakihi J. Bakili alichangia mifuko 100
ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo ya kijiji cha Mkutingome. Nao
Umoja wa Wachimbaji Wadogo katika mgodi wa Namungo ambao uko jirani na kijiji
hicho waliahidi kuchangia mifuko 50 ya saruji.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAMOSI, DESEMBA 31, 2016.
0 Comments