Na Jacquiline Mrisho –
MAELEZO.
Serikali imejipanga
kuwatoza kodi wakazi wanaomiliki maeneo yaliyopo mijini ambayo hayana hati wala
ofa kwa viwango vile vile ambavyo wakazi wenye hati wanatozwa.
Tamko hilo limetolewa
leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
William Lukuvi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya ulipaji wa
kodi za ardhi.
Waziri Lukuvi amesema
kuwa wizara hiyo inaendelea na ukaguzi wa ardhi ambapo mwanzoni ilianza na ukaguzi
wa mashamba yanayomilikiwa bila kuendelezwa lakini kwa sasa imegundulika kuwa kuna
maeneo makubwa mijini yasiyokuwa na hati yanamilikiwa na wananchi na
kusababisha eneo kubwa la ardhi kutumika bila kulipiwa kodi.
“Kwa muda wote huo
Serikali imekuwa haiwatozi kodi wananchi wanaomiliki maeneo mijini bila kuwa na
hati hivyo, kuanzia sasa Serikali kupitia wizara yangu itawatoza kodi watu wote
nchini wanaomiliki maeneo ndani ya miji hata kama hawana hati au ofa ili mradi
wana karatasi za mauziano ya ardhi,”alisema Lukuvi.
Ameongeza kuwa watu
wote waliopo mjini ambao wana ardhi lakini hawana hati wala ofa wapeleke
taarifa zao za maeneo wanayoyamiliki kwa
maafisa wateule wa ardhi kwenye halmashauri zao ili yaweze kujulikana ili
kuanza kulipiwa kodi.
Amefafanua kuwa kila
mwananchi lazima aende na kielelezo kinachoonyesha umiliki wake katika eneo
husika na akatamke mwenyewe ukubwa wa eneo alilonalo ili kama itatokea amedanganya ukubwa wa eneo lake na wizara
ikagundua basi eneo hilo lililozidi litamilikiwa na Serikali bila kulipa fidia
yoyote.
Aidha, Waziri Lukuvi
amesema kuwa kuanzia mwezi Julai mwaka huu wizara itaanza kuwatoza kodi
wananchi wote waliojenga mjini katika maeneo ambayo viwanja vyake havijapangwa
wala kupimwa kwani watu hao wanaishi mjini na wanatumia miundombinu ya umma
inayojengwa kwa kutumia kodi za wananchi.
“Ardhi ya Tanzania
inayotumika ni zaidi ya asilimia 70 lakini eneo linalolipiwa kodi halizidi
asilimia 11 na wengi wao wanaitumia isivyo rasmi na hawalipi kodi kwa Serikali
hivyo kila mtu mwenye ardhi awe na nyaraka rasmi au isiyo rasmi wote wanatakiwa
kulipa kodi ya ardhi na baada ya miezi 6 kutoka sasa, eneo ambalo halitakuwa
limesajiliwa litachukuliwa na kumilikiwa na Serikali,”alimalizia Lukuvi.
Ni lazima kuwatambua
watu wote wanaomiliki ardhi kisheria, kimila au kwa namna nyingine yoyote ili
kufahamu ardhi inamilikiwa na nani na inatumika kwa matumizi gani.

0 Comments