Na.
Immaculate Makilika na Lilian Lundo- MAELEZO.
Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe.
Yoweri Museveni ametoa wito wafanyabiashara wa Kitanzania kwenda kuwekeza
nchini Uganda.
Rais Museveni ametoa kauli hiyo leo
wakati alipotembelea viwanda vya Kampuni ya Bakhresa vinavyozalisha Unga
na Juisi vya Buguruni na Vingunguti jijini Dar es Salaam.
“Nawakaribisha
wafanyabiashara wa Kitanzania kuja nchini Uganda kuwekeza kwani kufanya hivyo
kutasaidia kuzalisha bidhaa, upatikanaji wa soko pamoja na ajira” alisema Rais
Museveni.
Kauli hiyo ya Rais Museveni
imetokana na mafanikio yanayotokana na Mwekezaji wa Kitanzania Said Salim
Bakhresa aliyewekeza nchini Uganda ambapo anamiliki Kiwanda cha kusanga ngano
nchini humo.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa
Mahusiano wa Kampuni za Bakhresa Hussin Sufiani amesema kwamba Kampuni hiyo iko
mbioni kuongeza uzalishaji wa unga wa ngano kutoka tani 1,100 hadi kufikia tani
2,000 kwa siku nchini Uganda.
Aidha, amesema kutokana na
uwekezaji wa Kampuni hiyo nchini Uganda jumla ya Waganda 650 wamenufaika na
ajira mbalimbali ambazo zinasaidia kuwapatia kipato.
Kwa upande wa Waziri wa Viwanda,
Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwaijage amesema kuwa Uganda na Tanzania
zimeingia makubakliano ya ushirikiano katika sekta mbalimbali
ikiwemo sekta ya viwanda.
Amesisitiza Watanzania wanaweza
kwenda kuwekeza nchini Uganda kwa vile nchi hiyo wanalima tani milioni 4 za
mahindi lakini wana uwezo wa kutumia tani milioni moja pekee, hivyo ni fursa
kwa wafanyabiashara wa Kitanzania kwenda kuwekeza nchini humo.
“Tunawahamasisha wafanyabiashara wa
Uganda na Tanzania kuwekeza katika nchi zao ili kuzalisha , bidhaa na ajira za
kutosha kwa wananchi” alisema Waziri Mwijage.
Waziri Mwijage alitoa Wito kwa
Watanzania kushiriki katika uchumi wa viwanda kwa kufanya uzalishaji wa bidhaa
zinazotumika viwanda mfanio kwa kulima matunda au mbogamboga.
Rais Yoweri Museveni aliwasili
nchini jana kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili ambapo akiwa nchini alifanya
mazungumzo na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
John Pombe Magufuli na kutembelea Viwanda vya Said Salim Bakhresa vya
Tazara na Vingunguti.

0 Comments