Wednesday 22 February 2017

SWEDY AIBUKA KIDEDEA UCHAGUZI MDOGO KITONGOJI CHA MAGOMENI B

 Diwani wa kata ya Magomeni Mwanaharusi Jarhuf(kushoto),na diwani wa kata ya Nianjema Abdul Pialla9kulia) wakimwinua mkono mwenyekiti mteule wa kitongoji cha Magomeni B Rajabu Swedy baada ya kutangazwa mshindi .(Picha na Mwamvua Mwinyi)
Mbunge wa jimbo la Bagamoyo,dk.Shukuru Kawambwa akimpongeza aliyekuwa meneja wa kampeni za chama cha mapinduzi(CCM)kitongoji cha Magomeni B kata ya Nianjema,alhaj Abdul Zahoro kwa ushindi alioupata,Rajabu Swedy na kuibuka na kura 441 dhidi ya vyama vya upinzani.

...........................................................................

Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo

MWENYEKITI mteule wa kitongoji cha Magomeni B, Nianjema, Bagamoyo,kupitia CCM, Rajabu Swedy amewashukuru wananchi wa kitongoji hicho kwa kumchagua kuwa mwenyekiti wa kitongoji hicho.

Aidha amesema amejipanga kuleta maendeleo na kusimamia kero ya miundombinu ya barabara, maji na umeme.

Swedy ameeleza kwamba hana chuki kwa wale ambao hawakumpigia kura kwani inaonyesha kukua kwa demokrasia .

Aliyasema hayo baada ya kutangazwa kuwa mshindi dhidi ya vyama vingine vitatu vya upinzani.

Alimpongeza mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi wilayani humo, alhaj Abdul Sharif kwa kumsimamia kwenye kampeni zake,mbunge, na viongozi wengine wa chama kwa kuhakikisha ushindi unapatikana.

Swedy alieleza kuwa kampeni na uchaguzi umeisha kilichobakia kwasasa ni kuchapakazi na kuwatumikia wananchi wote bila ya kujali itikadi za kisiasa.

"Nawashukuru wananchi wote walionipigia kura mimi,natambua wengine sio wananchama wa  CCM lakini ni kuguswa kwao kwa namna chama tawala kinavyotekeleza ilani yake"

"Na wahakikishia nitashirikiana na kila mmoja na nitawahudumia wananchi wote bila ya kuwabagua kwa kuleta maendeleo kwenye kitongoji hiki,” alisema Swedy .

Swedy akizungumzia wagombea wa vyama pinzani kushindwa kupewa ridhaa, alisema isiwe sababu ya kuwagawa wananchi ama kumbeza mshindi kwani huo unakuwa sio ukomavu wa kisiasa.

“Nitashirikiana nao katika suala la maendeleo ili kuhakikisha kitongoji kinapiga hatua kimaendeleo,” alisisitiza Swedy .

Alisema wananchi wasiwe na wasi wasi kwani kukichagua Chama Cha Mapinduzi ni kuchagua maendeleo hivyo wasubiri kuona utekelezaji kwa kushirikiana na chama, serikali,halmashauri pamoja na wadau. .

Swedy anasema kipaombele chake kikubwa ni kufungua njia mbalimbali zilizokuwa hazitumiki ili kuwarahisishia wakazi wa kitongoji hicho waweze kupita.

Aliyekuwa meneja wa kampeni katika kitongoji hicho, alhaj Abdul Sharif alishukuru wananchi kwa kumuamini na kukiamini chama kumsimamisha kupeperusha bendera ya CCM.

Alhaj Sharif alieleza, siasa za majukwaani zimemalizika, kikubwa ni kuwa na subira kungojea utekelezaji wa yale yaliyoahidiwa.

Awali msimamizi msaidizi wa uchaguzi kata ya Nianjema, Cezary Madasha, alimtangaza Swedy (CCM) kuwa mshindi kwa kupata kura 441 .

Huku Furaha Salehe wa(CHADEMA)akiwa na kura 332 ,Jumaa Chambo (CUF)  kura 140 na Wema Abdullah (ADC)  kura sita.

No comments:

Post a Comment