Random Posts

CCM Z'BAR YAZUNGUMZA MAZITO KUHUSU DAWA ZA KULEVYA

 Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai  akiwahutubia wanachama wa CCM katika Hafla ya Uwekaji wa jiwe la msingi Tawi la CCM Fuoni Michenzani.
 Baadhi ya Wana CCM wakila kiapo cha utii mara baada ya kukabidhiwa kadi za kujiunga na Chama pamoja na Jumuiya Zake katika hafla hiyo.
 Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai  akizindua jiwe la msingi katika tawi hilo la Fuoni Michenzani.
 Vijana wa Chipukizi wakimvisha sikafu ya heshima Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai  mara baada ya kuwasili katika hafla hiyo.
 Vijana wa sarakasi wakionyesha uwezo wao mbele ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Vuai Ali Vuai katika Hafla hiyo.

 NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

CHAMA Cha Mapinduzi  (CCM) Zanzibar kimewashauri  wanachama wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi  ndani ya chama na jumuiya  zake  kuhakikisha wanakemea vikali na  kuunga mkono kampeni  za kuthibiti  dawa za kulevya nchini ili kuwanusuru  vijana  wanaoathirika na janga hilo.

Ushauri huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Nd.Vuai Ali Vuai katika hafla ya  kuweka jiwe la msingi kwenye Tawi la CCM Fuoni Michenzani  Unguja, alisema dawa za kulevya ni sawa na bomu la maangamizi  linaloteketeza maelfu ya vijana  na kupoteza nguvu kazi nchini.

Vuai alieleza kuwa ni lazima kila mwanachama anayejiandaa kugombea nafasi ya uongozi ndani ya Chama hicho awe tayari kukemea na kupinga hadharani matumizi ya dawa za kulevya nchini kwa lengo la kuunga mkono juhudi zinazofanywa na viongozi wakuu wa Kitaifa akiwemo Mwenyekiti wa Chama hicho Dkt. John Pombe Magufuli na Makamo Mwenyekiti wake Dkt. Ali Mohamed Shein waliosimama imara kupambana vita hiyo.

Naibu Katibu Mkuu huyo alisisitiza kwamba kukemea matumizi ya dawa hizo kwa viongozi wa serikali na Chama sio maamuzi binafsi bali wanatekeleza ibara ya 155 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2015/2020 inayoeleza kwa kina mikakati ya kupambana na kuthibiti dawa hizo nchini kwa maendeleo ya wananchi wote.

Pia alisema ibara hiyo imeeleza hatua ya kuundwa kwa Tume ya kuthibiti dawa za kulevya pamoja na kuanzishwa kwa vituo vya matibabu ya  kuwatibu watu waliothirika na matumizi ya dawa hizo ikiwa ni hatua za kuwasaidia ambapo serikali zote mbili zimetekeleza matakwa hayo kwa kuruhusu taasisi binafsi kuanzisha vituo vya kurekebishia tabia (Soba house).

“Wanachama wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi ndani ya Chama na Jumuiya zetu lazima waonyeshe nia kwa vitendo ya kupambana na  dawa za kulevya na tukimuona mtu ana kigugumizi na muhali wa kukemea vitendo hivyo basi atakuwa hafai kuwa kiongozi kwani sote kwa sasa ni lazima tucheze wimbo mmoja katika mapambano haya”,. Alisisitiza Vuai na kuongeza kuwa  Dawa za kulevya ni Adui wa maendeleo ya nchi.

Hata hivyo aliwataka wanachama hao kutumia vikao halali kama vyenzo ya kujadili masuala ya shughuli za chama na kutafuta usuluhishi wa baadhi ya changamoto zinazojitokeza katika ngazi mbali mbali za chama hicho na kuepuka tabia za kujadili mambo ya chama nje ya vikao halali kwani kufanya hivyo kunatengeneza majungu na fitina.

Akizungumzia uchaguzi wa Chama unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni alisema kila mwanachama ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa hivyo watendaji watakaopewa majukumu ya kusimamia mchakato huo watekeleze majukumu yao kwa mujibu wa Katiba ili kila mwanachama mwenye nia apate haki yake kisheria.

“ Tunaingia katika uchaguzi wetu ndani ya Chama na Jumuiya kwa wale wenye nia ya kugombea Mjue kuwa katika mchakato wowote wa kisiasa hasa uchaguzi kuna kupata na kukosa hivyo tusije kugawanyika kwa kuwa pengine umekosa au amepata usiyempenda.”,  aliwasihi  Vuai wanachama hao.

Sambamba na hayo aliwapongeza viongozi na wanachama wa Tawi hilo kwa kutekeleza kwa vitendo matakwa ya kikatiba ya Mradi wa Awamu ya Tatu unaoagiza Chama na jumuiya kutekeleza kwa vitendo dhana ya Siasa na Uchumi kwa kujenga majengo ya kisasa yanayotoa fursa za kufanyika miradi ya kiuchumi inayowanufaisha wanachama wote.

Pamoja na hayo alitoa kadi kwa wanachama wapya waliojiunga na Chama na Jumuiya zake na kuwataka wafuate maelekezo na taratibu na miongozo ya kikatiba ndani ya chama hicho kwa lengo la kuleta ufanisi katika utelezaji wa shughuli za chama.

Akisoma risala mwanachama wa Tawi hilo Bi.Salhiya Ahmada alisema Tawi hilo limejengwa kwa msaada wa nguvu za wanachama kwa kushirikiana na baadhi ya wahisani ndani ya chama hicho ambao ni makada wa CCM akiwemo Makamo Mwenyekiti wa Chama hicho ambaye pia ni Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jimbo la Fuoni Kichama ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Dimani Juma Ali Juma alisema toka aingie madarakani amekuwa akitekeleza ilani ya CCM kwa kasi ambapo mpaka sasa tayari ametekeleza kwa kiasi kikubwa ahadi alizowaahidi wananchi ndani ya jimbo hilo.

Akizungumza Kada mkongwe wa CCM ambaye pia ni Mshauri wa Raisi wa Zanzibar katika masuala ya Utamaduni na Utalii Bw. Chimbeni Kheir Chimbeni  ambaye ni msimamizi mkuu wa Ujenzi wa Tawi hilio alitoa shukrani zake kwa wadau mbali mbali waliotoa michango yao kufanikisha ujenzi wa tawi hilo toka kununuliwa kwa kiwanja mpaka kusimamisha jengo hilo.


Katika hafla hiyo viongozi na wanachama mbali mbali walichangia fedha na taslim na wengine kutoa ahadi ya fedha zaidi ya milioni Tatu  ambapo naibu katibu Mkuu Vuai Ali Vuai kwa niaba ya Afisi Kuu Zanzibar aliahidi kuchangia shilingi milioni mbili na kugharamikia  baadhi ya matengenezo ya miundombinu ya jengo hilo.

Post a Comment

0 Comments