Na Mwamvua Mwinyi, Rufiji
Magari saba ya abiria yametekwa na watu wanaodhaniwa kuwa
ni majambazi huko barabara kutoka Dar es salaam kwenda mikoa ya Kusini
ya Lindi na Mtwara eneo la Mchukwi .
Kamanda wa polisi mkoani Pwani, Onesmo Lyanga alisema tukio hilo limetokea usiku wa march 22 kuamkia march 23 mwaka huu.
Akielezea tukio hilo, alisema kwamba watu hao waliweka
magogo katikati ya barabara ili kufanya wizi kwa abiria mbalimbali
waliokuwemo kwenye magari hayo.
Kamanda Lyanga alisema, baada ya magari kusimama
waliwashurutisha abiria kwa kuwapiga kwa mapanga na marungu na
kusababisha baadhi yao kujeruhiwa.
"Wameibiwa mali na fedha zao na baadhi yao kujeruhiwa kwa kupigwa "alisema .
Alibainisha kwamba, waliojeruhiwa walifikishwa Kituo cha afya Mchukwi kupata matibabu na kuruhusiwa.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, kwasasa wanawasaka wale wote waliohusika na tukio hilo.
Hata hivyo, kamanda Lyanga, alisema maeneo ya Mkuranga hadi
Utete na Rufiji yanaandamwa na uhalifu mbalimbali hivyo jeshi hilo
limejipanga kupambana na wahalifu.
Aliwataka wananchi kuacha kuwakumbatia wahalifu
wanaowafahamu kisa jirani ama ndugu bali washirikiane na jeshi hilo kwa
kuwafichua ili kuwachukulia hatua za kisheria.
Kamanda Lyanga alisema hawatakuwa na huruma kwa wahalifu
wanaotumia silaha, kupora, unyang'anyi kwani wanakosea amani raia walio
wema.
0 Comments