Na Jacquiline Mrisho –
MAELEZO.
Makamu wa Rais, Samia
Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla maalumu ya
kuwakaribisha viongozi wa Serikali itakayofanyika Machi 5 mwaka huu mkoani
Dodoma.
Hafla hiyo imeandaliwa
na Uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Dodoma na itafanyika mkoani humo katika
viwanja vya Nyerere (Nyerere Square) kuanzia saa 8 kamili mchana.
Afisa Habari wa Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa Dodoma, Jeremia Mwakyoma ameyasema hayo leo mjini Dodoma
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya ujio wa
viongozi hao katika Mkoa huo.
Mwakyoma amesema
viongozi wa Serikali kuhamia katika Makao Makuu ya Nchi ni sehemu ya
utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano hivyo Mkoa utawakaribisha rasmi
Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara
waliohamia kutoka Jijini Dar es Salaam.
“Tukio la viongozi wa
Wizara kuhamia Makao Makuu Dodoma ni la kihistoria ndio maana uongozi wa
Serikali ya Mkoa umeona ni vema kuweka utaratibu rasmi wa kuwakaribisha
viongozi hao,”alisema Mwakyoma.
Afisa Habari Mwakyoma
amewakaribisha wananchi wote wa Mkoa huo pamoja na Mikoa ya jirani kuhudhuria
kwa wingi kwenye hafla hiyo.
Mnamo Julai 25 mwaka 2016
katika maadhimisho ya siku ya mashujaa yalioadhimishwa mkoani Dodoma, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, John Pombe Magufuli alitangaza rasmi Serikali
kuanza mchakato wa kuhamia Dodoma ambapo ndipo yalipo Makao Makuu ya Nchi.

0 Comments