Random Posts

WANAWAKE NCHINI WATAKIWA KUJIWEZESHA KIUCHUMI, KIJAMII NA KISIASA.

  Jovina Bujulu- MAELEZO.
............................................
Wanawake nchini wametakiwa kujiwezesha kiuchumi, kijamii na kisiasa ili wapate fursa ya kushiriki katika maamuzi mbalimbali ambayo yatawaletea ukombozi wao na taifa.

Hayo yamesemwa jijini Dar-es-salaam na Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake nchini (TAMWA) Mama Edda Sanga alipokuwa akizungumzia mada kuhusu mapambano ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake.

Mama Sanga alisema kuwa unyanyasaji na ukatili dhidi ya wanawake kwa sasa umepungua kwasababu chama chake kimefanya juhudi kubwa ya kuwaelimisha wananchi kuhusu kutoa taarifa wanapoona kuna tatizo ili liweze kushughulikiwa mapema iwezekanavyo.

“Chama cha TAMWA kimevitumia vyombo vya habari kutoa hamasa, kuelimisha na kufanya utafiti wa kina kueleza ukatili huu, na hatimaye wahusika kufikishwa katika vyombo vya dola” alisema Mama Sanga.

Aliendelea kusema kuwa ingawa unyanyasaji na ukatili dhidi ya wanawake haujamalizika kabisa, kumekuwepo kesi ambazo zinafikishwa mahakamani na hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wanaofanya ukatili huo.

Mama Sanga alibainisha mkoa wa Mara kuwa ndio mkoa sugu kwa unyanyasaji na ukatili wa wanawake. Alitoa mfano wa Mama Neema Wandibe ambaye amefanyiwa ukatili wa kupindukia na usiokubalika na mumewe hivi karibuni kwa kummwagia maji ya moto, kwasababu alichuma mahindi mawili shambani na kuyachoma.

“Mkoa wa Mara umekubuhu katika unyanyasaji kwasababu ya kufuata mila na desturi kandamizi, ambazo zinamwona mwanamke kuwa ni mtu asiye na haki na sauti katika jamii” alisema Mama Sanga.

Mama Sanga amewataka wananchi na jamii kwa ujumla kushirikiana na vyombo husika katika kutoa taarifa na kwamba wanahitaji kujenga jamii yenye malengo kwa ajili ya kuondoa madhara ya unyanyasaji na ukatili wa wanawake.

Aidha, Mama Sanga amewataka wanawake kujitambua, kujiamini na kutoa elimu kwa watoto wao ili wakue katika hali ambayo ina umoja, na usawa katika kujiletea maendeleo yenye tija na ustawi wa jamii bora.

Katika kuthamini na kutambua mchango wa wanawake duniani Umoja wa Mataifa umetenga siku maalum ya wanawake wote ambayo husherekewa tarehe 8, Machi kila mwaka.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bibi Sihaba Nkinga alisema maadhimisho ya siku ya wanawake nchini yatafanyika katika ngazi ya Mkoa.

Katibu Mkuu huyo alisema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu “Tanzania ya viwanda, wanawake ni msingi wa mabadiliko ya kiuchumi”.


Zaidi ya hayo Katibu Mkuu huyo aliendelea kusema kuwa kauli mbiu hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia mazingira ya Tanzania, vipaumbele vya kimaendeleo na dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kufanya nchi kuwa ya viwanda na uchumi wa kati.

Post a Comment

0 Comments