Jovina
Bujulu – MAELEZO.
Maadhimisho
ya Siku ya Wanawake Duniani, ni hatua muhimu kwa wanawake kujipambanua na
kufanya tathmini jinsi wanavyoshiriki katika ujenzi wa taifa kiuchumi, kijamii
na kisiasa.
Serikali
imeweka mikakati na mipango mbalimbali yenye lengo la kumkomboa na kumuinua
mwanamke kiuchumi.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto, mama
Sihaba Nkinga hivi karibuni alipokuwa akizungumzia mipango na mikakati mbalimbali
iliyofanywa na Serikali katika kumkomboa na kumuinua mwanamke kiuchumi.
Pamoja
na kuwa wanawake wengi wameamka na wanajishughulisha katika masuala mbalimbali
ya kiuchumi, Serikali pia inahakikisha inawawezesha ili waweze kufikia malengo
yao katika masuala ya kujiinua kiuchumi na kuondokana na dhana ya utegemezi.
“Serikali
ina mipango mbalimbali katika kuhakikisha kuwa wanawake wamewezeshwa kiuchumi,
ikiwa ni pamoja na kuanzisha benki ya Wanawake ambayo moja ya majukumu yake ni
kuhakikisha wanawake wanapata mikopo kwa kuzingatia viwango wanavyoweza kulipa”
alisema mama Nkinga.
Aliitaja
mikakati mingine kuwa ni pamoja na kuwa na mfuko wa maendeleo ya wanawake
ambapo wanawake wanapewa mikopo yenye riba nafuu ambayo wanamudu kuilipa.
Aidha,
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameweza kuwasaidia wanawake katika
masuala ambayo yamekuwa yakiwasumbua kwa muda mfefu kama vile umiliki wa ardhi.
Kupitia elimu hii kwa sasa wanawake wanaruhusiwa kumiliki ardhi kisheria na
kuondoa utata kuhusu suala hili.
Pamoja
na mikakati hiyo, Serikali imeenelea kushirikiana na wadau kuhakikisha kuwa
vikwazo mbali mbali vya mitaji na mikopo vinaondolewa ili kuhakikisha kuwa
wanawake wengi wanapata fursa ya kukopa na kulipa kwa muda hivyo kuwa huru
kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.
“Idadi
kubwa ya wakina mama wapo kwenye ujasiriamali na viwanda vidogo vidogo hivyo Serikali
imekuwa ikitoa elimu kwao na kuwahimiza kukopa kwenye vyombo na taasisi za
fedha kwa sababu huko wanakopa kulingana na uwezo wao na hii itawasaidia
kufanikisha shughuli zao za ujasiriamali“ aliongeza mama Sihaba .
Aliwaasa
wanawake kuachana na sekta isiyo rasmi na badala yake wajikite katika sekta
rasmi maana huko kuna uzalishaji mkubwa ambao utawapatia soko la nje na
aliwataka kuboresha bidhaa zao ili wawe tayari katika ushindani mkubwa zaidi
wakati nchi yetu ikielekea katika uchumi wa viwanda.
Akizungumzia
fursa na mlingano wa ajira kati ya wanawake na wanaume alisema kuwa upande wa
ajira wote wanawake na wanaume wana nafasi sawa na kinachozingatiwa ni vigezo
na sifa za waombaji wa ajira.
Katibu
Mkuu huyo aliendelea kusema kwa sasa hakuna kazi za wanaume peke kwani upo uhalisia juu ya ushiriki wa wanawake wengi
katika kazi za uhandisi, ukandarasi na udaktari.
Alitoa
wito kwa wanawake, jamii na watanzania kwa ujumla kuitumia siku hii kutoa
hamasa kwa wanawake na kuangalia nafasi yao katika jamii kipindi hiki ambapo Tanzania
inaelekea katika uchumi wa kati na viwanda.
Ili
kufikia azma ya uchumi wa viwanda, ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha anadumisha
Umoja wa nchi yetu na Utanzania wetu kwa kuwashirikisha wanawake, kwa kutoa
elimu na kuwapa nafasi ili watoe mchango wao ipasavyo katika kuinua uchumi wa
nchi.
Aidha,
mama Nkinga alihimiza jamii kusimamia watoto wa kike na kuhakikisha wanapewa
haki inayostahili ili nao wafike mahali waweze kutoa mchango wao kwa taifa.
Siku
ya wanawake duniani huadhimishwa kila ifikapo tarehe 8, Machi kwa shughuli
mbalimbali kama vile maandamano na hotuba, pia wanawake hutumia nafasi hiyo
kutathmini mafanikio ya shughuli zao za maendeleo, changamoto zilizopo na
kuweka mikakati ya utatuzi wa changamoto hizo. Kauli mbiu ya mwaka huu inasema “Tanzania
ya viwanda, wanawake ni msingi wa mabadiliko ya kiuchumi.”

0 Comments