Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Plan
International- Tanzania, Jorgen Haldorsen akikata keki ikiwa ni ishara ya
kuadhimisha kuzaliwa kwa shirika hilo. Maadhimisho ya miaka 80 ya kuzaliwa kwa
shirika hilo yamefanyika jana Jijini Dar es Salaam katika Makao Makuu ya Ofisi
hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Plan
International- Tanzania, Jorgen Haldorsen akizungumza na watumishi (hawapo
pichani) juu ya maadhimisho ya miaka 80 ya kuzaliwa kwa shirika hilo jana
Jijini Dar es Salaam katika Makao Makuu ya Ofisi hiyo.
Baadhi ya watumishi
wa shirika la Plan International wakifurahi kwa pamoja wakati wa kuadhimisha
kuzaliwa kwa shirika hilo. Maadhimisho ya miaka 80 ya kuzaliwa kwa shirika hilo
yamefanyika jana Jijini Dar es Salaam katika Makao Makuu ya Ofisi hiyo.
....................................................
Na Jacquiline Mrisho –
MAELEZO.
Shirika lisilokuwa la
Kiserikali la Plan International limeadhimisha miaka 80 tangu kuzaliwa kwake Mwaka
1937 likiwa na lengo la kutetea na kusimamia
haki za Watoto pamoja na usawa wa kijinsia.
Maadhimisho hayo yamefanyika jana Duniani kote
katika nchi ambazo shirika hilo linafanya kazi, kwa Tanzania maadhimisho
yamefanyika katika Mikoa yote ambayo ina ofisi za shirika ambapo wafanyakazi
waliofanya kazi zaidi ya miaka 20 walitambuliwa.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo-
Tanzania, Jorgen Haldorsen amesema shirika la Plan limesaidia kwa kiasi kikubwa
kuimarisha maisha ya Watoto na wasichana wengi duniani tangu kuzaliwa kwake na
litaendelea kutimiza malengo yaliyowekwa ya kuhakikisha haki za watoto
zinalindwa na usawa wa kijinsia unapatikana ikiwa ni njia moja wapo ya kuchochea
maendeleo ya nchi husika.
”Leo shirika letu linatimiza miaka 80 tangu
kuanzishwa kwake, ni safari ndefu tena yenye mafanikio makubwa ingawa bado kuna
mengi ya kufanya ili kuhakikisha haki za watoto na wasichana zinalindwa
ulimwenguni kote kama yalivyokuwa malengo ya John-Langdon-Davies ambaye ndiye
muanzilishi wa shirika hili,”Alisema Haldorsen.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa
ingawa shirika hilo linakua na kubadilika kulingana na muda lakini lengo la kuhakikisha
watoto na wasichana wanayafikia malengo yao waliyojipangia haliwezi kubadilika
kwani wanatambua kuwa unyanyasaji wa watoto wa kike na uvunjwaji wa haki za
watoto ndiyo sababu moja wapo ya kukithiri kwa umasikini katika nchi nyingi.
Haldorsen amefafanua,ili kutatua
changamoto hizo wamejikita katika kutoa Elimu na ulinzi kwa watoto ambapo amekiri
kuwa kazi hiyo imewezekana kwa sababu ya ushirikiano mkubwa wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wafadhili pamoja na wadau mbalimbali.
Aidha, mnamo miaka ya 1980 wakati
shirika likiadhimisha miaka 50 ya kuzaliwa kwake ilikuwa ni mwaka muhimu kwa
shirika kwani ndio siku ambayo walitambuliwa rasmi na Shirika la Kimataifa la
Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) kama moja ya shirika la Kimataifa
linaloshughulikia Watoto na Wasichana.
Kwa Tanzania shirika hilo limenza tangu mwaka 1991
likisaidia watoto pamoja na jamii nzima katika kuboresha Afya, Elimu Ulinzi na
Ajira.Mwaka 2000 shirika lilianzisha Ofisi katika Wilaya tano za Vijijini na
moja ikiwa mjini na mwaka 2011 shirika lilianzisha shughuli zake za kupeleka
misaada katika Mikoa 14 Tanzania Bara na Visiwani.
Mikoa hiyo inajumuisha Dar es Salaam, Mtwara, Lindi, Ruvuma, Morogoro,
Dodoma, Iringa, Rukwa, Kigoma, Geita, Mwanza, Mara na Visiwa vya Zanzibar.



0 Comments