Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Shirika lisilokuwa la kiserikali
la Plan International mwaka 2016 lilifanya utafiti na kugundua kuwa
nafasi ya watoto wa kike ulimwenguni haionekani machoni pa watu.
Hatua hiyo inatokana na sababu
zinazoonesha kuwa takwimu zinazowahusu watoto wa kike ziko nyuma ya
wakati, hazijakamilika na muda mwingine tafiti zake hazifanyiwi
utekelezaji.
Nchini Tanzania imeonekana hakuna
takwimu sahihi zinazoonyesha uhalisia wa changamoto anazozipata mtoto
wa kike kutokana na ndoa za utotoni, hivyo kupelekea thamani ya mtoto wa
kike kushuka katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo ambapo madhara
yake yanaonekana baadae akiwa mtu mzima.
Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi wa
Mtoto kutoka Shirika la Plan International–Tanzania, Jane Mrema anasema
kiwango cha ndoa za utotoni kwa Tanznia kimefikia asilimia 36 ambacho ni
kiwango kikubwa zaidi ya kiwango cha Dunia ambacho ni asilimia 34 na
kwa hesabu za kimkoa ni asilimia 59 kwa kila mkoa.
“Hiyo ndio sababu kubwa
iliyopelekea Shirika letu kuungana na Serikali pamoja na mashirika
mengine kufanya utafiti huo wenye lengo la kufahamu vitu vinavyopelekea
ndoa za utotoni pamoja na madhara yake baada ya ndoa hizo
kutokea,”anasema Bi. Jane.
Utafiti huo umefanyika kwa
ushirikiano wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto na Mashirika yasiyo ya Kiserikali yakiwemo ya Shirika la kutetea
haki za watoto (Plan International), Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF),
Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), Shirika linalohusiana na
Utafiti na maendeleo ya Afya ya Wanawake (FORWARD) pamoja na Shirika la
Utafiti juu ya Kupunguza Umasikini (REPOA).
Baada ya utafiti huo kukamilika,
iliandaliwa ripoti ambayo ilizinduliwa mnamo Machi, 2 mwaka huu na
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu, ripoti inayojulikana kama Ripoti ya Utafiti wa Visababishi na
Madhara ya Ndoa za Utotoni Nchini Tanzania.
Ripoti hiyo imeonyesha kuwa umasikini ndio sababu kubwa inayopelekea kuwepo kwa ndoa za utotoni.
Baadhi ya mikoa ambayo wananchi
walihojiwa wakati wa utafiti wamekubali kwa nguvu zote kuwa fedha
zinazolipwa kwa ajili ya mahari ndizo zinazowasababisha kuwaoza watoto
wao wakiwa bado wadogo.
Utafiti huo unaonesha mkoa wa
Mara wananchi asilimia 59 wanakubalina na majibu ya utafiti huo ambapo
mkoa wa Dar es Salaam asilimia 56, mkoa wa Dodoma asilimia 53, mkoa wa
Lindi asilimia 52 na mkoa wa Tabora asilimia 51.
Sababu nyingine ya ndoa za
utotoni ni mtazamo wa tamaduni, mila na desturi baina ya jamii
mbalimbali kuhusu miaka ya mtoto wa kike anayetakiwa kuolewa, unyago,
ukeketaji pamoja na ngoma za asili zinazopelekea watoto kuozwa mapema.
Tafiti hizo zinaonyesha kwamba
maeneo ya vijijini asilimia 18 ya wanawake wamekeketwa wakati Mijini ni
asilimia 7 na Mikoa inayoongoza ni Manyara asilimia 81, Dodoma asilimia
68, Arusha asilimia 55, Singida asilimia 43 na Mara asilimia 38.
Aidha, asilimia 24 ya waliohojiwa
mkoani Shinyanga na asilimia 20 ya mkoani Tabora wamesema mikoa hiyo
ina kiwango kikubwa cha ndoa za watoto walio na umri chini ya miaka 18.
Utafiti huo pia umegundua kuwa
ukosefu wa elimu unapelekea wasichana kuingia kwenye ndoa wakiwa bado
wadogo kiumri hii inatokana na kushindwa kuendelea na masomo baada ya
kumaliza elimu ya msingi.
Kutokana na utafiti huo,
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Plan International- Tanzania, Jorgen
Haldorsen anasema “Matokeo ya utafiti huo yanawapa mwongozo wa kujua
sehemu zilizoathirika zaidi ili kuweka nguvu za kutosha na kufahamu
namna mbalimbali za kutumia kuwafikia waathirika hao”.
Akizindua ripoti hiyo, Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema
kuwa anapozindua ripoti hiyo ni dhahiri anapinga kwa vitendo ndoa na
mimba za utotoni kwani ni changamoto kwa maendeleo ya Tanzania.
“Tunataka Tanzania kuwa nchi ya
viwanda, lakini hatutaweza kuwa na nchi yenye viwanda wakati watoto 36
katika kila watoto 100 nchini wanaolewa kabla ya kufikia umri wa miaka
18 na watoto 27 wa kitanzania wanapata mimba kabla ya umri huo, hili ni
tatizo kubwa ambalo athari zake zitaonekana baadae”anasema Waziri Ummy.
Katika kuhakikisha ndoa hizo
zinakoma, Waziri Ummy ameanza kutumia marekebisho ya Sheria ya Elimu
yaliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo June
2016 ambayo yanakataza mtu yoyote kumuoa mtoto wa shule ya Msingi au
Sekondari kwani ni kosa la jinai lenye adhabu ya miaka 30 jela.
Pia, Waziri Ummy amewataka
Maafisa Maendeleo ya Jamii wa kila Halmashauri kupita nyumba kwa nyumba
kuwaibua wazazi wanaofanya vitendo hivyo na kuwasilisha taarifa hizo
sehemu husika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sheria hiyo.
Waziri Ummy ameyaahidi mashirika
hayo ya kutetea haki za watoto kuendelea kushirikiana nao katika kuwapa
semina wazazi juu ya athari za ndoa za utotoni, kuwapa watoto elimu ya
afya ya uzazi pamoja na kuboresha mazingira ya shule ili kuwawezesha
wasichana kupata hamasa ya kwenda shule.
Kwa upande wa viongozi wa dini
Mchungaji Cistus Mallya pamoja na Sheikh Swedi Twaibu wanasema mtoto
lazima apate malezi mazuri kutoka kwa wazazi ili aweze kufahamu mabaya
na mazuri na aweze kujiepusha na vitendo viovu vikiwemo vya kudanganywa
na kuingia katika mapenzi wakiwa na umri mdogo.
Viongozi hao wamemuomba Waziri
Ummy kuangalia utaratibu wa kuwalea watoto wanaoishi katika mazingira
magumu ili nao baadae waje kuwa wanawake wanaoweza kuleta maendeleo
katika taifa lao.
Akiwakilisha vijana wa kike, Catherine Kapilima amesema ndoa za utotoni uhathiri afya, elimu na maendeleo ya mtoto wa kike.
Aidha, Catherine amesema kuwa
wazazi kupewa elimu pekee haitoshi kwani kuna wengine ambao sio waelewa,
hivyo ni jukumu la Serikali kuweka nyumba ambazo ni salama kwa ajili ya
kuwapokea na kuwapatia huduma muhimu watoto wa kike wanaokimbia kutoka
kwa wazazi wasiokuwa waelewa.
Ni wakati muafaka sasa Wadau wote
wa Maendeleo nchini kwenda zaidi Vijijini kuwasaidia wanawake na
wasichana waliopo huko kwani ndio maeneo yenye waathirika wengi wa ndoa
na mimba za utotoni ikilinganishwa na mijini.
Ikiwa Dunia inakarabia
kuadhimisha siku ya wanawake duniani mnamo Machi, 8 mwaka huu, Serikali,
wadau pamoja na wananchi waungane kwa pamoja kuzuia ndoa za utotoni ili
kuandaa wanawake imara katika miaka ijayo.
Tunaamini kuwa watoto wa kike wa
sasa ndio wanawake wa kesho hivyo ni vema kuwaandaa kuwa wanawake bora
wenye kuweza kujitegemea na watakaoweza kuleta maendeleo katika nyanja
mbalimbali za kiuchumi nchini.

0 Comments