Timu ya taifa ya
Tanzania chini ya miaka 17, Serengeti Boys, imeibuka na ushindi mnono
wa mabao 3-0 dhidi ya vijana wenzao wa Burundi katika mchezo wa kirafiki
uliopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera.
Katika mchezo huo
ambao Serengeti Boys inautumia kwa ajili ya maandalizi yao kabla ya
kwenda Gabon kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana
chini ya miaka 17, ulishuhudiwa mpaka mapumziko timu hiyo ikiwa mbele
kwa mabao 2-0.
Mabao hayo yalifungwa
na Muhsin Makame dakika ya 20 na Nickson Kibabage, huku Yohana Mkomola
akimalizia msumari wa mwisho dakika ya 72 kwa njia ya mkwaju wa penalti
na kukamilisha idadi hiyo ya mabao 3-0.
Baada ya leo
kumalizana na Burundi, Jumatatu ijayo kikosi cha Serengeti Boys
kinatarajiwa kucheza mchezo wa mwisho wa kirafiki jijini Dar es Salaam
dhidi ya Ghana kabla ya kwenda Morocco kuweka kambi ya mwisho ya
kujiandaa na michuano hiyo ya vijana.
Katika michuano hiyo itakayoanza kuunguruma Mei 14, mwaka huu, Serengeti Boys imepangwa Kundi B sambamba na timu za Mali,
Niger na Angola. Kama Serengeti Boys itafanya vizuri kwenye michuano
hiyo, basi itajikatia tiketi ya kwenda kushiriki michuano ya Kombe la
Dunia chini ya miaka 17 itakayofanyika hapo baadaye nchini India.

0 Comments