Waziri Kairuki (wa pili kutoka kushoto) akifanya usafi
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) leo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha
siku ya wanawake duniani. Kushoto ni Mkurugenzi wa Uuguzi wa Muhimbili, Agness
Mtawa. Kutoka kulia wa kwanza ni Katibu wa Umoja wa Wanawake katika Wilaya ya
Ilala, Joyce Ibrahimu Mkaugala na Zuhura Mawona wakifanya usafi Leo katika
hospitali hiyo.
Waziri Kairuki akizungumza na kinamama waliojifungua
watoto kabla ya kuwapatia zawadi ya nguo za watoto, pampazi na sabuni.
Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais Menejementi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa
Angellah Kairuki akikabidhi vitanda 10
na magodoro 10 kwa Mkurugenzi wa Uuguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),
Agness Mtawa.
Mkurugenzi wa Uuguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH), Agness Mtawa akimshukuru Waziri Kairuki baada ya kupokea msaada wa
vitanda na magodoro leo.
Hospitali ya Taifa Muhimbili –MNH- leo imeungana na wanawake
wengine ulimwenguni kote kuadhimisha siku ya wanawake Duniani kwa kufanya usafi
katika maeneo mbalimbali ya hospitali hiyo.
Zoezi hilo limeongozwa na Mbunge wa Vitimaalum mkoa wa Dar
es salaam Mheshimiwa Angellah Kairuki kwa niaba ya Umoja wa Wanawake wa Chama
cha Mapinduzi –UWT- mkoani humo.
Mheshimiwa Kairuki ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais Utumishi na Utawala Bora amesema katika kusheherekea siku ya wanawake
Duniani UWT imeona ni vema wakashiriki
katika shughuli mbalimbali za kijamii ili kuonesha dhamira ya dhati kwamba CCM
inawajali wananchi wake bila kujali itikadi ya chama.
‘’ Sisi tumekuja hapa Muhimbili kushiriki na nyinyi katika kuadhimisha
siku hii kwa kufanya usafi bila kujali itikadi ya chama kwani Hospitali hii
inahudumiwa wananchi wote , pia siku hii
ya leo tunatoa msaada wa vifaa mbalimbali vya watoto na wenzetu wengine wameenda katika Hospitali
zingine wote tukiwa na lengo moja’’. Amesema Waziri Kairuki.
‘’Msaada tuliotoa ni vitanda kumi, magodoro kumi , mashuka na vifaa vingine mbalimbali vya watoto
zikiwamo nguo ,sabuni na Pampers lengo
ni kuunga mkono juhudu za serikali za kuboresha huduma za afya hususani afya ya mama na mtoto na kuhakikisha hakuna
mgonjwa anayelala chini kwa kukosa kitanda’’ . Amesema Mheshimiwa Kairuki.
Akipokea msaada wa vitanda hivyo Mkurugenzi wa Huduma za
Uuguzi na Ukunga wa MNH Agnes Mtawa amewashukuru UWT kwa msaada walioutoa
ambao amesema umekuja wakati muafaka kwani utasaidia katika kutekeleza majukumu
yao .
Hata hivyo Mkurugenzi Mtawa amewakumbusha wauguzi kuendelea
kufanya kazi kwa kufuata maadili na kusisitiza kuwa kazi hiyo inahitaji kujitoa
na kuwa na moyo wa huruma .
Siku ya wanawake Duniani huadhimishwa kila Machi nane ambapo
kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘’ Tanzania ya Viwanda , Wanawake ndio msingi wa
mabadiliko ya kiuchumi .





0 Comments