Naibu Waziri wa
Fedha na Mipango Mhe. Ashatu Kijaji (Mb) akisisitiza kuhusu jitihada
zinazofanywa na Serikali katika kutatua changamoto ya deni la Shirika la Ugavi
wa Umeme Tanzania (Tanesco) kwa kuendeleza juhudi za kutumia nishati mbadala ya
Gesi badala ya Mafuta mazito katika kuendesha mitambo ya Uzalishaji wa umeme, katika
kikao na Wakurugenzi Watendaji wanaoziwakilisha nchi zao katika Benki ya Maendeleo
ya Afrika (AfDB), ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa
Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)(kushoto) akiongoza Mkutano wa
Wakurugenzi Watendaji wanaoziwakilisha nchi zao katika Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB), katika kufanya tathmini ya maendeleo ya Miradi inayofadhiliwa na
Benki hiyo, ambapo Wakurugenzi hao waliipongeza Tanzania kwa kutekeleza miradi
kwa ufanisi. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji kutoka Afrika ya Kusini Bi. Mmakgoshi
Lekhethe aliyeongoza ujumbe wa Wakurugenzi Watendaji wengine 12 (hawapo
pichani), katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa
Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji
kutoka Afrika ya Kusini Bi. Mmakgoshi Lekhethe (kulia) wakipeana mikono baada
ya kumalizika kwa mkutano wa tathmini ya maendeleo ya Miradi inayofadhiliwa na
Benki hiyo nchini Tanzania, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini
Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (wanne kulia) na Mkurugenzi Mtendaji
kutoka Afrika ya Kusini Bi. Mmakgoshi Lekhethe (wa tano kushoto) wakiwa katika
picha ya pamoja na Wakurugenzi Watendaji wanao ziwakilisha nchi zao katika
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), baada ya kumalizika kwa mkutano wa
tathmini ya maendeleo ya Miradi inayofadhiliwa na Benki hiyo nchini Tanzania,
katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa Wakalimani
aliyeambatana na Wakurugenzi Watendaji wanao ziwakilisha nchi zao katika Benki
ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), akisalimiana kwa bashasha na Naibu Waziri wa
Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), (kulia) baada ya kumalizika kwa
mkutano wa tathmini ya utekelezaji wa miradi
inayofadhiliwa na Benki hiyo nchini Tanzania, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha
na Mipango, Jijini Dar es salaam, ikiwa ni ishara njema kwa Taifa kwa kuwa
walipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali za kupambana na umaskini.
........................................
Na Benny Mwaipaja, WFM
Naibu Waziri Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji
(Mb) amesema Serikali inaendelea kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB) katika kuhakikisha miradi yote ikiwemo ile inayofadhiliwa na Benki hiyo
inatekelezeka kwa ufanisi Mkubwa.
Dkt. Kijaji ameyasema hayo alipokutana na Wakurugenzi Watendaji 12
wanaoziwakilisha nchi zao katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), katika
Mkutano uliofanyika Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dar es salaam, baada ya ujumbe
huo kutembelea miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Benki hiyo hapa nchini.
“Madhumuni makubwa ya ziara ya Wakurugenzi watendaji wa Benki ya
AfDB waliokuja nchini tangu Februari 25,
ni kukaa pamoja na Serikali ili kujadiliana kuhusu sera na mipango mikakati ya maendeleo, lakini pia kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa
kupitia ufadhili wa Benki ya hiyo” Alifafanua Dkt. Kijaji.
Wakurugenzi hao ambao ndio watoa maamuzi katika Benki hiyo, wametembelea
miradi ya maji Zanzibar na kwa upande wa Tanzania Bara wametembelea mradi wa
kufua umeme wa Sokoine substation uliopo Manispaa ya Ilala.
Katika Mkutano huo, Serikali ya Tanzania imeendelea kuiomba Benki
ya AfDB kuharakisha kazi za upembuzi yakinifu na
hatimaye kutoa fedha ili utekelezaji wa miradi ya Maendeleo uanze mapema kwa
kadri inavyowezekana.
Miradi
hiyo ni pamoja na ule wa North – West grid wa kusafirisha Nishati ya Umeme
kutoka Shinyanga hadi Mbeya kupitia Kigoma Katavi na Rukwa. Mradi utakaowezesha
Mikoa ya Ukanda wa Magharibi kupata Nishati ya uhakika ya umeme na kufungua
fursa za Maendeleo mbalimbali yakiwemo ya ujenzi wa Viwanda vidogo na vya kati.
Kwa
kushirikiana na Benki hiyo ya AfDB mradi mwingine unaofanyiwa kazi ili kupata fedha
za kuanza kuutekeleza ni ule wa kujenga
barabara ya Nyakanazi, kupitia Kibondo, Kasulu hadi Manyovu, kwa kiwango cha
lami na iwapo mradi huo ukipatiwa fedha na kukamilika kwa wakati kutasaidia
kuchochea biashara ya wakazi wa maeneo hayo pamoja na Nchi ya Burundi.
Kwa upande wa Wakurugenzi
Watendaji wa AfDB wanaoziwakilisha nchi zao, wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji
kutoka Afrika ya Kusini Bi. Mmakgoshi Lekhethe, wameipongeza Serikali ya Awamu
ya Tano chini ya Rais
John Pombe Joseph Magufuli kwa ufanisi katika Nyanja zote ikiwemo ya kupambana
na umaskini.
Wageni hao wamefurahishwa na namna Tanzania invyotekeleza miradi
inayofadhiliwa na Benki hiyo, kwa kuwa kila walipopatembelea, wameona uthabiti
na umadhubuti wa miradi, jambo ambalo limewaongezea hamasa ya kufanya kazi kwa
karibu na nchi hiyo.
Wameitaka Serikali kuendelea kulishughurikia suala la deni la
Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania-TANESCO, ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji kwa
lengo la kuchochea maendeleo ya nchi mijini na Vijijini.
Naibu Waziri Dkt. Kijaji amebainisha kuwa ipo mikakati iliyowekwa
na Serikali ya kutatua suala la deni hilo kwa kuwa tatizo kubwa lilikuwa
matumizi ya Mafuta ya dizeli katika kuendeshea mitambo TANESCO.
Aidha alisema kuwa kwa sasa upatikanaji wa Nishati ya Gesi katika
maeneo mbalimbali ya Tanzania, utasaidia katika kuendesha mitambo hiyo badala
ya Mafuta hivyo kutatua suala la deni hilo linalo likabili Shirika na hatimaye
kutimiza ndoto ya watanzania ya kuimarika kwa uchumi utakao chochewa na Sekta
hiyo.
No comments:
Post a Comment