Na Jacquiline Mrisho
– MAELEZO.
Wanawake na vijana
wanaopewa mikopo na Serikali kupitia Halmashauri ya Mji wa Ifakara mkoani
Morogoro wamekumbushwa kupeleka marejesho kwa wakati ili kuwapa fursa na
wananchi wengine kupata mikopo hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa
Halmashauri hiyo, Christopher Msimbe ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu nafasi ya vijana
walemavu waliomaliza mafunzo kupitia Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE)
unaoratibiwa na Shirika la Plan International.
Msimbe amesema pamoja
na kuwepo kwa changamoto mbalimbali, Halmashauri inatambua nafasi ya vijana
katika jamii hasa vijana wenye ulemavu na ndio sababu wanawakumbuka katika
fursa nyingi zinazokuja katika Halmashauri hiyo kutoka kwa wadau mbalimbali.
“Katika Halmashauri
yetu tumebahatika kupata mradi wa YEE unaowashirikisha hata vijana wenye
ulemavu, mradi huo unalenga kuwapatia mafunzo ya ufundi vijana ili waweze kujitegemea
hivyo sisi kama Serikali tumetoa jumla ya shilingi 4,000,000 kwa vikundi viwili
vya vijana wenye ulemavu ili waweze kuinua shughuli zao,”alisema Msimbe.
Amefafanua kuwa
Halmashauri zote nchini zinatakiwa kutenga fedha kwa ajili ya kuwapatia mikopo vijana
na wanawake ili kuwasaidia kujikwamua kimaisha kwa kuendelezea biashara zao
lakini asilimia kubwa wamekuwa hawapeleki marejesho kwa wakati na kusababisha
Halmashauri kushindwa kutoa mikopo kwa watu wengine.
Nae, Mwenyekiti wa
Mtaa wa Kiungwile “A” iliyopo wilayani Kilombero Mkoa wa Morogoro, Emmanuel
Sama amesema mradi huo umewasaidia vijana wengi kwa sababu kabla ya mradi huo
vijana walikuwa wakizurura mitaani bila kazi yoyote pia vijana walemavu
walikuwa wakikaa ndani bila kujua hatima yao.
“Mtaani kwangu nina
vijana watano waliopewa mafunzo na shirika hili ambao wamefanikiwa kuunda
kikundi chao kijulikanacho kama ‘Baraka Farmers Group’ ambacho kinatumia elimu
waliyoipata pamoja na mkopo wa shilingi 1,500,000 kutoka katika Halmashauri
yetu kujiendeleza kiuchumi, nawashkuru vijana hawa kwani wanatumia vizuri fursa
waliyopewa na kurejesha fedha walizokopeshwa kwa wakati,”alisema Sama.
Sama ametoa rai kwa
wananchi wanaopewa mikopo na Serikali hasa wananchi wasio na ulemavu ambao
wanaweza kufanya kazi kwa uhakika kurejesha fedha za mikopo kwa wakati ili
Halmashauri iweze kuendelea kuwasaidia wananchi wengine na watakaokaidi
watachukuliwa hatua stahiki ili warudishe fedha hizo.
Mradi
huo wa miaka mitatu umeanza mwaka 2015 hadi 2018 unatekelezwa kwa ushirikiano
wa mashirika ya VSO, CCBRT, VETA, UHIKI, CODERT pamoja na Serikali ya Tanzania
huku ukiratibiwa na Shirika la Plan International chini ya ufadhili wa Umoja wa
Nchi za Ulaya (EU).

0 Comments