Kamishna wa Bima, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima
Tanzania Bw. Baghayo Abdallah Saqware akiongea na waandishi wa habari kuhusu
mwelekeo wa sekta ya Bima nchini na mikakati ya kuendeleza na kupanua shughuli
za bima nchini, leo Jijini Dar es salaam. Kushoto ni Meneja Mawasiliano wa
mamlaka hiyo Bw. Eliezer Rweikiza
Meneja TEHAMA, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania
(TIRA) Bw. Aron Mlaka akiwaeleza waandishi wa habari mikakati ya mamlaka hiyo
ya kuongeza na kupanua matumizi ya Teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama)
katika kuboresha huduma zao. Kushoto ni
Naibu Kamishna wa Mamlaka hiyo Bw. Juma Makame.
Mkurugenzi wa
Masoko na Utafiti TIRA Bi. Adelaide Muganyizi akifafanua jinsi Mamlaka hiyo
inavyotoa elimu kwa Umma pamoja na umuhimu wa Bima wakati wa mkutano na waandishi
wa habari, leo Jiji Dar es saam. Kushoto ni Naibu Kamishna wa Mamlaka hiyo Bw.
Juma Makame.
(Picha na Georgina
Misama)
..........
Na:
Lilian Lundo – MAELEZO
Mamlaka ya Usimamizi
wa Bima Tanzania (TIRA) imejizatiti kurudisha thamani ya huduma za bima kwa kubadilisha
baadhi ya sheria na kanuni za bima pamoja na kutengeneza mfumo wenye kutoa tija kwa Wananchi, Serikali pamoja na Kampuni
za Bima nchini.
Hayo yamesemwa na
Kamishna wa Bima, Baghayo Saqware alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu
ya namna mamlaka hiyo ilivyojipanga kurudisha thamani ya bima kwa wananchi na
makampuni ya bima hapa nchini, leo Jijini Dar es Salaam.
Baghayo Saqware
amesema kwamba moja ya kanuni na sheria zitakazoboreshwa ni pamoja na kupeleka
biashara ya bima (Insurance business – risks) nje ya nchi badala ya kutumia
makampuni ya ndani.
“Tutaweka kanuni
itakayolazimisha Kampuni za bima hapa nchini kuongeza mitaji au kutengeneza mfuko wa pamoja au mfumo
wa makampuni kushirikina kimtaji ili kuweza kuandikisha na kubakisha sehemu kubwa
au biashara yote ya bima nchini,” alifafanua Saqware.
Aliendelea kwa kusema
kuwa utawekwa utaratibu wa kisheria utakaohakikisha waingizaji wa mizigo kutoka
nje ya nchi wanakatia bima za mizigo yao kupitia kampuni za bima nchini.
Aidha amesema kwamba
ikibidi mamlaka hiyo itabadilisha sheria ya bima nchini ili wafanyabiashara
wanaoagiza bidhaa kutoka nje ya nchi (import
goods) iwe ni lazima kukatia bima nchini
ili kuongeza mapato ya kodi (VAT) pamoja na bima (Premium Levy).
Katika kurudisha
thamani ya huduma ya bima kwa wananchi mamlaka hiyo itahakikisha makampuni yanayotoa
huduma ya bima yanatoa huduma stahiki
kwa wateja wa bima pamoja na kuhakikish malalamiko ya wateja yanayofikishwa katika mamlaka husika yanashughulikiwa kwa
wakati.
Aidha, katika kupanua
shughuli za bima mamlaka hiyo iko katika hatua za mwisho za kukamilisha bima ya
kilimo, mifugo pamoja na bima za watu wenye kipato cha chini (Micro-insurance)
pamoja na kukamilisha utekelezaji wa sera ya Taifa ya Bima.
Vile vile inapanua
matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) kwa kutumia utaratibu
wa kusajili na kutoa leseni za biashara
ndani ya siku saba hadi thelathini, aidha mfumo huo utaondoa tatizo la bima
bandia za vyombo vya moto pamoja na kuhakiki uhalali wa stika za bima kwa
walionazo.
Nae, Meneja Tehama
TIRA, Aron Mlaki amesema kwamba mfumo huo wa Tehama utamuwezesha mwananchi
kupata maelezo ya bima yake kupitia
intanenti na meseji za kawaida ambapo kwa upande wa message za kawaida ataandika
neno ‘STIKA’ likifuatiwa na namba ya
Stika na kuituma kwenye namba 15200 baada ya hapo atapokea taarifa za bima
yake.



0 Comments