Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na baadhi ya watanzania wanasoma na wale wanaoishi nchini Mauritius baada ya kuzungumza nao kwenye hoteli ya Meridien nje kidogo ya mji wa Port Louis, Machi 22, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na baadhi ya watanzania waishio
na wale wanaosoma nchini Mauritius kwenye hoteli ya Meridien,nje kidogo
ya Mji wa Port Louis Machi 22, 2017.Kulia ni Waziri wa Fedha wa
Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohammed.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya watanzania waishio nchini Mauritius na maofisa wa serikali ya
Tanzania wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza
nao kwenye hoteli ya Meridien, nje kidogo ya mji Port Louis Machi 22,
2017.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
........................................
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amewataka Watanzania wanaoishi nje ya nchi wazingatie sheria za Taifa
husika na kamwe wasijihusishe na biashara haramu ya dawa za kulevya.
“Vita ya dawa
za kulevya ni kubwa, hata hivyo Serikali tunaendelea kupambana nayo. Nchi
ilikuwa inapoteza vijana ambao walikuwa wamejiingiza katika biashara haramu ya
dawa za kulevya. Nawaomba msithubutu kuingia huko mtafungwa,” amesema.
Waziri Mkuu
ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Machi 22, 2017) wakati akizungumza na Umoja wa
Watanzania wanaoishi nchini Mauritius katika mkutano alioutisha kwenye hoteli
ya Meridien mjini Port Louis.
Amesema
katika kudhibiti biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya Serikali iliamua
kuunda Mamlaka
ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na inafanya
kazi vizuri. “Na tutakamata kila mtu anayejihusisha na biashara hiyo bila
kujali cheo, uwezo na mamlaka aliyonayo,”.
Amesema
mamlaka hiyo inafanyakazi ya kutafuta wazalishaji, watumiaji na wafanyabiashara,
lengo likiwa ni kuokoa vijana ambao wameshindwa kutimiza ndoto zao kutokana na
madhara waliyoyapata baada ya kutumia dawa za kulevya.
Katika hatua nyinngine, Waziri Mkuu
amewataka Watanzania hao walioko nchini Mauritius kujenga mshikamano wa pamoja
na wawe na uzalendo na nchi yao. Pia wawe mabalozi wazuri wa kutangaza vivutio
vya Taifa.
Amesema ni vema wakatumia fursa walizonazo
katika kutafuta wawekezaji na kuwashawishi waje nchini na kuwekeza kwenye sekta
mbalimbali zikiwemo za viwanda, uvuvi, nishati na utalii.
Kwa upande
wake, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohammed
amewaomba Watanzania hao wazidishe mshikamano miongoni mwao kwa kuwa umoja wao
ndiyo nguzo yao.
“Mko hapa kwa ajili ya
kutafuta elimu na wengine mnafanya kazi, shughuli ambazo zitawasaidia kuboresha maendeleo yenu na
Taifa kwa ujumla, hivyo nawaomba mzingatie kilichowaleta,” amesema.
Naye
Mwenyekiti wa muda wa Umoja wa Watanzania waishio nchini Mauritius, Bw. Donald
Kongwa ambaye ni Ofisa wa benki ya Standard Chaetered nchini Mauritius
amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba kipato wanachokipata watakitumia kwa
kuwekeza Tanzania kwa lengo la kukuza uchumi wa Taifa.
Aidha,
amesema wanaunga mkono na kupongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu
ya Tano katika kujenga uchumi wa
viwanda, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, ujenzi wa miundombinu ya kisasa,
ununuzi wa ndege pamoja na kuimarisha uwajibikaji na nidhamu kwa watumishi wa
umma.
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU,
JUMATANO,
MACHI 22, 2017.
0 Comments