Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano
na Mazingira), Mhe. January Makamba akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Pangani Bi.
Zainab Abdallah mara baada ya kutembelea kijiji cha Buyuni na kuongea na
wananchi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano
na Mazingira), Mhe. January Makamba (Mb.) akiongea na Bi. Tatu Rajab mmoja wa
wafanyakazi katika Kiwanda cha kutengeneza chumvi cha Sea Salt. Waziri Makamba
alifanya ziara kiwandani hapo kuangalia changamoto za mazingira.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano
na Mazingira), Mhe. January Makamba (kushoto) akiwa katika kikao cha majumuisho
na Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Maggid Mwanga mara baada ya kukamilisha ziara
katika Wilaya hiyo.
Na
Lulu Mussa Saadani
- Pwani
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba amesema katika
jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake Ofisi yake
imeandaa mradi utaonufaisha shule za msingi katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa
Pwani.
Akiwa Wilayani Bagamoyo
Waziri Makamba amesema kuwa, moja ya changamoto kubwa ya Wilaya ya Bagamoyo ni
ukame unaotokana na athari za mabadiliko ya Tabianchi, uliopelekea kupanda kwa
kina cha bahari na kusababisha visima vilivyochimbwa pembeni mwa miji na fukwe
za bahari kufukiwa na maji na chumvi.
"Ofisi ya Makamu ya
Rais imeamua kuisadia Wilaya ya Bagamoyo kuchimba visima kumi na saba (17)
virefu kwenye maeneo ambayo yameathirika na kupanda kwa kina cha maji na maeneo
yenye ukame mkubwa" Makamba alisisitiza.
Takribani kila kisima
kitagharimu kiasi cha Shilingi Milioni Hamsini na Ofisi ya Makamu wa Rais pia
itaandaa mfumo wa kuvuna maji katika shule tano mradi utakao gharimu takribani
Milioni mia moja sabini.
Katika hatua nyingine
Waziri Makamba alitembelea Kiwanda cha Sea Salt kilichopo Saadani, Wilaya ya
Bagamoyo kuona namna kiwanda kinavyofanya kazi kwa kuzingatia Sheria ya
Mazingira ya mwaka 2004.
Waziri Makamba ambaye amewasili
Mkoani Tanga kujionea hali ya mazingira na changamoto za uhifadhi pia ametembelea
Wilaya ya Pangani na kukagua mradi wa ujenzi wa Ukuta wa Pangani.
Waziri Makamba, amemtaka mkandarasi
anayejenga ukuta wa mto Pangani kampuni ya ( DEZO CIVIL CONSTRUCTION L.TD )
kukamilisha ujenzi wa ukuta kwa kipindi cha muda wa miezi kumi, kama mkataba
unavyoonyesha na kuzingatia ubora. Ujenzi huo wa sehemu ya ufukwe wa kaskazini ambao una urefu
wa mita 950 ambazo kati yake mita 550 zipo katika ujenzi wa awali utagharimu
kiasi cha shilingi za kitanzania Bilioni 2.4
Kwa upande wake Mkuu wa
Wilaya ya Pangani Bi Zainab Abdalah amemuomba Waziri Makamba kutuma timu ya
wataalamu kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu kwa fukwe pekee iliyoko katika
maeneo ya Tanga DECO ambayo imeathirika kwa kiasi kikubwa na athari zitokanazo
na mabadiliko ya Tabia nchi na haipo katika bajeti kwa mwaka huu wa fedha.
Ziara ya kikazi wa Waziri
Makamba leo imeingia siku ya pili na ametembelea Kijiji cha Buyuni ambapo pia
alifanya mazungumzo na wakazi wa eneo hilo.



0 Comments