Benny Mwaipaja-WFM,
Dodoma
Mikoa mitatu ya Tanga,
Morogoro na Iringa, imenufaika na kiasi cha shilingi bilioni 6.5 zilizotolewa
kama mkopo na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) tangu benki hiyo ianzishwe
mwaka 2015.
Kauli hiyo imetolewa
leo Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu
Kijaji, wakati akijibu swali na msingi lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu,
Mhe. Felister Aloyce Bura, aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itaanza kutoa
huduma kwa wakulima wadogo wadogo wa mkoa wa Dodoma.
Dkt. Kijaji ameeleza
kuwa hadi kufikia mwezi Desemba, 2016, TADB imetoa mikopo ya jumla ya shilingi
6,489,521,120 kwa ajili ya kutekeleza miradi ishirini (20) ya kilimo katika
mikoa hiyo mitatu ya Iringa, Morogoro na Tanga.
“Sambama na utoaji
mikopo, Benki inatoa mafunzo kwa wakulima ambapo hadi sasa vikundi 336 vya
wakulima wadogowadogo vyenye jumla ya wanachama 44,400 wamepatiwa mafunzo hayo
katika mikoa hiyo mitatu” aliongeza Dkt. Kijaji
Amesema kuwa Benki hiyo
inatarajia kuanza kutoa huduma hiyo kwa wakulima wadogowadogo wa Mkoa wa Dodoma
na mikoa mingine jirani wenye sifa.
“Benki imepata nafasi
kwa ajili ya kufungua ofisi katika jengo la PSPF mjini Dodoma na itakabidhiwa
ofisi hiyo mwezi Julai, 2017, baada ya mkandarasi kukamilisha ujenzi wa jengo
hilo” Alisisitiza Dkt. Kijaji
Dkt. Kijaji amesema
kuwa tayari Benki hiyo imemwandikia barua Katibu Tawala wa mkoa wa Dodoma ili
kuomba aipatie miradi mizuri ya kilimo ambayo mkoa unapendekeza Benki iifikirie
katika zoezi la kutoa mikopo itakayoanza kutolewa mwishoni mwa mwaka 2017.

0 Comments