Na Judith Mhina - MAELEZO
Waziri Mkuu mstaafu wa Awamu ya
Kwanza Dkt Salim Ahmed Salim amesema ili
muungano wa Tanganyika na Zanzibar uweze kudumu na kuimarika hatuna budi
kuelezea mafanikio yalitopatikana na pia kutafuta ufumbuzi wa kero chache
zilizopo.
Dkt, Salim Ahmed Salim amesema
hayo leo jijini Dar Es salaam wakati wa mahojiano na Idara ya Habari – MAELEZO
kuhusiana namaadhimisho ya miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika
hizi karibuni.
Warizi huyo msataafu amekiri
kwamba Watanzania wana haki ya kujivunia muungano huu ambao ni wa asili
kutokana na mahusiano yetu ya kindugu hata kabla ya Muungano. “Mahusiano ya kindugu baina ya Wananchi wa
Tanganyika na Zanzibar ni ya miaka mingi ambapo watu wake wamekuwa
wakitembeleana na kuoana.
Aidha, mahusiano hayo yameonekana katika masualoa ya
kijamii kama vile lugha, dini n.k.
Dkt Salim ameeleza kwamba, walichokifanya
Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Shekh Abeid
Amani Karume ni kuweka uwazi juu ya mahusiano ya watu wa Tanganyika na Zanzibar
duniani hususan kwa wale ambao hawajui asili ya watu wa pande hizo mbili.
“ Jambo hili la Muungano kudumu miaka 53 linashangaza
watu wengi duniani, hasa kwa dhana kwamba nchi za kiafrika zina matatizo, na sio
rahisi kuelewana. Jambo kubwa linalofanikisha
kudumu kwa Muungano wetu ni umoja,
upendo na mshikamano. Tumekuwa tukuweka wazi mafanikio na pale penye changamoto
hukaa pamoja na kuzungumza ili kuyapatia ufumbuzi.”
Akizungumzia suala la vijana
kushika madaraka Serikalini, Dkt Salim amesema “Hii si jambo geni kwani mimi ndiye kijana wa kwanza ambaye
niliaminika nikiwa mdogo sana miaka 22 na kuteuliwa kuwa Balozi nchini Misri.
Kazi hii haikuwa ndogo lakini niliifanya kazi kwa kujiamini na kwa uadilifu
mkubwa huku nikipata maelekezo kutoka kwa viongozi wangu wakuu (Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar).
Hivyo napenda kuchukua nafasi
hii kutoa wito kwa Watanzania wenzangu hususan vijana wanaoaminiwa na Taifa
katika umri mdogo kushika uongozi wakubali nafasi hizo kwa kuwa bado wana nguvu
ya kuweza kulitumikia Taifa letu. Lakini wasisahau kuwasikiliza viongozi
waliowapa nafasi hizo, na ushauri wa wazee ni muhimu sana. Aidha, wajue kuwa nafasi
za uongozi wanazomepewa kuwawakilisha Watanzania zilete maendeleo ya kweli.
Akielezea mustakabali wa
maendeleo ya nchi, Dkt Salim alitolea mfano wa vijana wa Afrika ya Kusini
ambapo hivi katibu alikwenda kushiki moja ya mikutano viongozi wa nchi za
Afrika. hivi Amesema, vijana wa Afrika ya Kusini hawataki kusikia lolote zaidi
ya mambo yanayowahusu wao na maisha yao. Hawajui kama kuna watu wamepigania
uhuru na hatimaye ukombozi wa nchi yao.
Wao hilo si kipaumbele kwao, wanachotaka ni maendeleo ambayo yatagusa maisha
yao.
“Hivyo ni vema Serikali zetu
zilivyoamua kuelekeza nguvu katika viwanda vidogo vya kati na vikubwa, kwa
sababu malighafi tunazo za kutosha ila tulikosa mbinu za kuongeza thamani ya malighafi
zetu. “Nataka nikuhakikishie tuko kwenye njia sahihi ili kuwafanya vijana walio
wengi washiriki katika kulijenga Taifa na kupata ajira ambazo zitawafanya
waishi kwa furaha na matumaini,” Asema Dkt Salim.
Akijibu swali, kuhusiana na lipi
la kujivunia kutokana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Dkt Salim amesema :
“ Umoja wetu ndio uliotufikisha miaka 53, tusingekuwa wamoja tungegawanyika na
Muungano ungekuwa mashakani.
Angalia
idadi kubwa ya Watanzania sasa ni wale waliozaliwa baada ya Muungano ambao
hawajui lolote kuhusu Muungano.
Tuna Jukumu kubwa la kuendeleza
elimu ya historia kwa vizazi vya sasa na vijavyo waelewe na kudhamini kazi
zilizofanywa na waasisi wetu wa Muungano Mwalimu Nyerere na Shekh Karume. Mfano
mzuri ni Taifa la China ambalo vijana wengi hawakuwahi kumuona Mao SeThung,
lakini wanamjua kutokana na historia wanayoelezwa na matunda yake ambayo wanayaona.
Pili, Watanzania tusibaguane kama alivyosema Mwalimu Nyerere kwamba
dhambi ya ubaguzi haiwezi kuishia hapo unapombagua mtu, itaendelea kwa mwingine
na mwingine na mwisho Taifa litagawanyika.
Aidha, Dkt Salim amesema kwamba Taasisi ya Mwalimu Nyerere
itaendelea kutoa elimu ya umuhimu wa muungano ambao ni tunda la umoja na
mshikamano barani Afrika, hususani Tanzania ambao wanahitaji kuwa na elimu ya
uraia.
Mwisho alimalizia kwa kutoa wito
kwa Watanzania kuuenzi na kudumisha muungano wetu ulioanzishwa na Waasisi wetu Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere na Shekh Abeid Amani Karume.

0 Comments