NAIBU KATIBU MKUU WA CCM Z’BAR
DKT. ABDALLA JUMA SAADALA MABODI AKIWAPUNGIA MKONO WANANCHI NA WANACHAMA WA
CHAMA HICHO MARA BAADA YA KUINGIA KATIKA MAKAAZI YA WANA TUMBATU GOMANI.
KUNDI MAALUM LA VIJANA WA CHAMA
HICHO WANAOTUMIA ZANA ZA ASILI KUSHEREHESHA WAKIONGOZA MSAFARA WA ZIARA HIYO
KWA KUTOA BURUDANI MBALI MBALI.
MAMIA YA WANACCM WALIOJITOKEZA
KUMPOKEA NAIBU KATIBU MKUU WA CCM Z’BAR DKT. ABDALLA JUMA SAADALA MABODI MARA BAADA YA KUWASILI KATIKA KISIWA HICHO.
MSAFARA WA NAIBU KATIBU MKUU WA CCM Z’BAR DKT. ABDALLA JUMA SAADALA MABODI PAMOJA NA VIONGOZI,WANACHAMA NA WATENDAJI WA
CCM WA KISIWA HICHO WAKIWA KATIKA ARDHI YA TUMBATU KUELEKEA KATIKA WADI YA
TUMBATU GOMANI NDANI YA KISIWA HICHO.
NI NAIBU KATIBU MKUU WA CCM Z’BAR DKT. ABDALLA JUMA SAADALA MABODI PAMOJA NA VIONGOZI VIONGOZI WA MKOA WA KASKAZINI UNGUJA NA
MAAFISA WA AFISI KUU ZANZIBAR WAKIWA KATIKA BANDARI NDOGO YA MKOKOTONI KUELEKEA
KISIWA CHA TUMBATU KATIKA MWENDELEZO WA ZIARA YA UIMARISHAJI WA HALI YA KISIASA YA CCM KATIKA WILAYA YA KASKAZINI “A”.
NAIBU KATIBU MKUU WA CCM Z’BAR DKT. ABDALLA
JUMA SAADALA MABODI AKIWAHUTUBIA NA KUWAPA NASAHA WANACHAMA WA CCM, VIONGOZI, WATENDAJI
WA JUMUIYA NA CHAMA WA NGAZI ZA MASHINA HADI MKOA KATIKA TAWI LA CCM GOMANI.
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM
Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala Mabodi amesema kuwa hakuna Chama wala
taasisi yoyote ya kisiasa inayoweza kuzuia Chama hicho kisisimamie utekelezaji wa Ilani
Uchaguzi ya mwaka 2015/2020 kwa wananchi wa Visiwa vya Zanzibar.
Msimamo huo ameutoa katika
mwendelezo wa ziara zake za kuimarisha uhai wa Chama huko katika Kisiwa Cha
Tumbatu Wilaya ya Kaskazini “A” kichama, wakati akizungumza na wanachama,
viongozi na watendaji wa CCM Wadi ya Tumbatu Gomani.
Alisema kila jambo
linalofanywa ama kutekelezwa na CCM lipo katika nyaraka za kimiongozo na
kisheria ambazo ni Katiba ya Chama, Ilani na miongozo ya maadili na Uchaguzi
tofauti na vyama vingine vya kisiasa vinavyoongozwa na matakwa binafsi ya watu wachache.
Pia alisema misingi hiyo ndio
chimbuko la Ukomavu wa kisisa na Demokrasia iliyotukuka ndani ya CCM, na inawajengea ujasiri viongozi wa chama
hicho kusimama popote kujenga hoja imara
za kuinada ilani ya chama kwani wanajua kuwa hakuna wa kuzuia utekelezaji wake.
Mwanasiasa huyo ambaye
amefanya ziara katika kisiwa hicho kidogo cha Tumbatu kilichopo Wilaya ya
Kaskazini “A” Mkoa wa Kaskazini Unguja, kwa mara ya kwanza toka alipoteuliwa
kushika nafasi hiyo hivi karibuni, aliwasihi Wana CCM hasa wazee kuendelea kuwa
karibu na taasisi hiyo ili waweze kutoa ushauri na maoni yao juu ya masuala
mbali mbali ya uongozi na utendaji.
Alieleza kwamba Chama hicho
bado kinaendelea kutekeleza kwa vitendo ahadi zote zilizoahidiwa katika
uchaguzi Mkuu uliopita bila ya kujali itikadi za kisiasa, kidini na
kikabila ili wananchi wote waweze
kunufaika na matunda ya serikali inayotokana na Chama Tawala.
Dkt. Mabodi aliwambia
wananchi hao kwamba wanatakiwa kuthamini na kulinda miradi mbali mbali inayotekelezwa
na serikali kwani imetokana na nguvu zao ambao waliichagua kwa kura nyingi CCM
isimamishe serikali yenye maono na utu wa kuwatumikia wananchi kwa vitendo.
Hata hivyo alifafanua
kwamba CCM haina muda wa kurumbana na kushughulikia hoja dhaifu za wapinzani na
badala yake inaenda mbio kusimamia kuwakumbusha viongozi na taasisi za umma
zenye wajibu wa kushughulikia mipango ya maendeleo na ustawi wa jamii, kuona
inakamilika kwa wakati.
“ CCM ni chama
kinachotokana na ASP na TANU vilivyokuwa vyama vya wakulima na wakwezi na
vikaikomboa nchi na kutuachia matunda haya, hivyo ni lazima tuyalinde na
kuyatetea kwa vitendo.
Pia puuzeni kwa nguvu zote uzushi na sera
zizisokuwa na maana juu ya maisha na maendeleo ya nchi, kwani hazina lengo la
kutufikisha pale tunapopataka zaidi ya kutugawa na ndio maana CCM inapinga kwa
nguvu zote dhana za migogoro na utengano.”alieleza Dkt. Mabodi na kuwataka wana
CCM kuendelea kulinda Amani na Utulivu wa nchi huku wakiendelea kufanya kazi
kwa bidii za kujiongezea kipato.
Akitoa ufafanuzi juu ya
Uchaguzi wa Chama hicho unaoendelea kwa ngazi ya Matawi kuchukua fomu
aliwaagiza Makatibu na Manaibu Katibu wa Chama na jumuiya zingine kuahakikisha
wanafuata taratibu zilizowekwa ili kila mtu mwenye nia ya kugombea apate nafasi
hiyo.
“ Kama nikibaini kwamba
kuna mizengwe ama makundi ya kutuharibia uchaguzi ngazi yeyote kwanza watu
tuliowapa majukumu watawajibu pia uchaguzi huo nitawashauri wenzangu ikibidi
ufutwe na kufanyika tena kwani tunahitaji watu wenye uwezo na uchungu na
chama”. Alisema Naibu katibu huyo.
Aliwataka wanachama
kuhakikisha wanachagua viongozi wenye sifa na wanaokubalika katika jamii ambao
watajenga timu ya kukiletea ushindi na heshima chama hicho katika uchaguzi mkuu
ujao.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa
wa Kaskazini Unguja, Haji Juma Haji akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu huyo
alisema kwamba CCM imepitia katika vipindi tofauti vya kiutawala hivyo bado ipo
imara kutokana na uzoefu wake unaotokana na ridhaa halali za wananchi.
Mapema Katibu wa CCM Wilaya ya Kaskazini “A” alisema kwamba Serikali imeweza kutekeleza kwa ufanisi Ilani
ya Uchaguzi ya Taasisi hiyo kwa vitendo kwani imeleza mageuzi makubwa ya
kiuchumi na kijamii, ambayo ni kuwapatia
Umeme, vituo vya afya vya kisasa, skuli na miradi mbali mbali ya Uvuvi
inayoharakisha maendeleo ya wakaazi wa
Tumbatu.
Aidha alilalamikia vyombo
vya Ulinzi hasa Jeshi la Polisi ndani ya Wilaya hiyo kushindwa kutoa
ushirikiano kwa viongozi wa CCM hasa pale wanapohujumiwa na watu wanaosadikiwa
kuwa ni wapinzani.
Akizungumza mwanachama wa
CCM wadi ya Tumbatu Bi. Nali Makame Ngwali alikishauri Chama hicho kuwapatia
nafasi za kutembea sehemu mbali mbali nje ya kisiwa hicho kwa lengo la kwenda
kutembea na kujifunza masuala mbali mbali hasa ya ujasiria mali na mafunzo ya
kujiajiri wenyewe.
Wanachama wa CCM na
wananchi wa Kisiwa hicho wamejitokeza kwa wingi kumpokea kwa shangwe kiongozi
huyo toka alipotua katika Pwani ya kisiwa hicho.







0 Comments