Wakati kamati ya Sheria,Katiba na Hadhi za Wachezaji
ikitaraji kutoa maamuzi muda wowote kuanzia sasa juu ya hatma ya pointi
tatu na mabao matatu waliyopewa klabu ya Simba,baada ya klabu ya Kagera
Sugar kuwasilisha malalamiko TFF wakipinga maamuzi ya kupokwa pointi
tatu na kamati ya saa 72 leo hii uongozi wa Simba umeweka bayana juu ya
swala hilo.
Akiongea mbele ya waandishi wa Habari leo hii katika makao
makuu ya klabu,Mkuu wa idara ya Habari na mawasiliano wa klabu ya
Simba,Haji Manara amesema kwamba hakukuwa na haja ya kamati ya
Katiba,Sheria na Hadhi za Wachezaji kuitisha kikao kwa ajili ya kujadili
marejeo ya shauri la Kagera Sugar kwa madai kuwa haina uhalali wa
kufanya jambo hilo.
Manara alisema kwamba uongozi wa Simba unashangaa kuona
mtuhumiwa anaitwa kwenye Review au mwamuzi wa nne ambaye hata haandiki
ripoti kutoa ushahidi kwenye kamati jambo ambalo ni kinyume na kanuni na
halijawahi kutokea.
“Licha ya kikao kutokuwa na uhalali juu ya swala hilo lakini
pia kwenye suala la Review hakupaswi kuitwa mashahidi wapya sasa
nashangaa kuona wanahojiwa watu ambao katika maamuzi ya awali
hawakuwepo”alisema Manara.
Aidha alisema kwamba anashangaa kuona maswala ya klabu ya
Simba ambayo yamewasilishwa kwenye kamati za TFF yanashindwa kupatiwa
ufumbuzi tena ya muda mrefu lakini kwenye swala la Kagera Sugar kwa
sababu lina maslahi kwa upande wao wameamua kulifanya haraka haraka.
Hata hivyo alisema kwamba msimamo wao kama uongozi ni kuona
TFF inafanya uhalali na kuendelea kutenda haki kwa kila klabu na endapo
watashindwa kufanya uhalali juu ya Review ya Kagera Sugar wanaamini
swala hilo litafika mbali kwani wamechoka kuonewa na TFF iliyo chini ya
Raisi Jamali Malinzi.


0 Comments