Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji
wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72 imeipa Simba SC pointi
tatu na mabao matatu kutokana na rufaa waliyoikatia Kagera Sugar kwa
kumtumia beki Mohammed Fakhi akiwa ana kadi tatu za njano katika mechi
baina ya timu hizo Aprili 2, mwaka huu.
Katika mchezo huo ambao Kagera
Sugar walishinda mabao 2-1 Uwanja wa Kaitaba, wanadaiwa kukiuka kanuni
kwa kumchezesha Fakhi, beki wa zamani wa Simba badala ya mchezaji huyo
kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano alizopata mfululizo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Ahmed
Yahya amewaambia Waandishi wa Habari usiku wa April 13, 2017 kwamba
Kamati ilibaini ni kweli Kagera Sugar walifanya kosa hilo la kikanuni na
adhabu yake ni kupokonywa ushindi.
Kwa ushindi huo, Simba sasa
inafikisha pointi 61 baada ya kucheza mechi 26, wakiendelea kuongoza
Ligi Kuu Tanzania bara mbele ya mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 56
wakiwa wamecheza mechi 25.
Ikumbukwe Simba iliwasilisha
malalamiko ikitaka ipewe ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kutokana
na Kagera Sugar kumchezesha Fakhi akiwa na kadi tatu za njano katika
mechi yao namba 194 iliyofanyika Aprili 2, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini
Bukoba.
Katika kikao chake awali Ijumaa
iliyopita, Kamati baada ya kupitia malalamiko hayo, iliahirisha shauri
hilo hadi leo (April 13, 2017) kujipa muda wa kufuatilia baadhi ya
vielelezo kuhusu malalamiko hayo.
“Malalamiko yaliletwa kwetu na
timu ya Simba baada ya kufungwa na Kagera Sugar 2-1 kwenye uwanja wa
Kaitaba, Simba walileta malalamiko kwamba kuna mchezaji mmoja wa Kagera
Sugar Mohamed Fakhi alicheza mchezo huo wakati akiwa na kadi tatu za
njano jambo ambalo ni kinyume na taratibu zetu kwa mujibu wa kanuni zetu
za ligi,” alisema mwenyekiti wa kamati ya saa 72 wakati akitangaza
uamuzi uliofikiwa na kamati yake.
“Tulikaa kikao cha kwanza siku ya
tarehe 7 April, 2017 tukajadili, bahati mbaya siku hiyo hatukufanikiwa
kufikia mwisho kwa sababu tulikuwa tunakosa baadhi ya taarifa ambazo
zinaendana na maamuzi ambayo tungeweza kuyafanya kwa hiyo tulijipa muda
hadi leo na tumefanikiwa kuzipata taarifa ambazo tulikuwa tunazitafuta
na jioni hii tumefikia maamuzi.”
“Kutokana na nyaraka tulizonazo
imethibitika kwamba, mchezaji huyu ambaye anaitwa Mohamed Fakhi alipata
kadi ya njano kwenye mchezo kati ya Kagera Sugar na Mbeya City, akapata
kadi nyingine ya njano kwenye mchezo kati ya Kagera Sugar na Majimaji na
pia akapata kadi ya njano kwenye mchezo kati Kagera Sugar na African
Lyon.”
“Baada ya kupata malalamiko haya,
watu wa Kagera Sugar walikuja juu na kusema kwamba, mchezaji wao
alipewa kadi kwenye mchezo kati ya Kagera Sugar na African Lyon na huo
ndio utata uliotufanya tutafute ushahidi kuona kwamba hicho kitu
kilitokea. Tumepata taarifa na kamati imeridhia kwamba hiki kitu
kilitokea na kutokana na hilo, mchezaji huyo alikuwa nje ya sheria 37
(14) na adhabu yake ipo kwenye sheria yetu ambayo inasema kwamba (timu
itakayotumia mchezaji ambaye ana kadi tatu za njano, basi itabatilishiwa
matokeo na kunyang’anywa ushindi. Timu pinzani itapewa ushindi wa
pointi na magoli matatu).”
Kwa hali hiyo, naomba nitangaze rasmi kwamba, kamati imefikia maamuzi hayo na taratibu zingine zitafuata kuhusiana na hilo.
Tumechukua muda mrefu kutoa
maamuzi kwa sababu ya hali ilivyokuwa, kwamba upande wa pili walikuwa
wanasema rekodi zao hazioneshi hivyo kwa hiyo ilibidi tutafute rekodi za
ziada ndiyo maana tumechukua muda mrefu kutoa maamuzi ya suala hili.
Vinginevyo tungetoa maamuzi siku ya tarehe 7 tulipopata malalamiko haya.


0 Comments