Mkuu
wa kituo cha
polisi Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Evarest Makalla,
akipokea printa kutoka kwa Ofisa mahusiano wa Kampuni ya TanzaniteOne,
Halfan Hayesh ambapo makampuni
hiyo ilitoa msaada wa printa moja na kompyuta mbili zenye thamani ya
shilingi milioni 1.5 kwa ajili ya kusaidia kituo hicho.
Kampuni
ya TanzaniteOne imetoa msaada wa
kompyuta mbili na printa moja kwa ajili ya kituo cha polisi Mirerani
Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara zitakazowasaidia kuandikia
nyaraka na shughuli za polisi.
Msaada
huo wenye thamani ya sh1.5 milion utawezesha askari polisi kuandika maelezo ya kazi,
mambo ya utendaji na upelelezi wa kesi mbalimbali, tofauti na hapo awali
walikuwa wanaenda mitaani kuandika kwenye ofisi binafsi za raia.
Ofisa
mahusiano wa kampuni ya TanzaniteOne, Halfan Hayesh, akizungumza wakati
akikabidhi msaada huo, alisema lengo lao ni kuwawezesha polisi ambao ni wadau
wa usalama wa eneo hilo wanaofanya kazi kwa ukaribu.
Hayesh
alisema wametoa kompyuta mbili mpakato (Lap top) aina ya Lenovo na print aina
ya HP, ambazo zitawasaidia askari polisi kuweka kumbukumbu zao ipasavyo tofauti
na hapo awali walipokuwa wanaenda kufanya kazi uraiani.
Alisema
haikuwa jambo zuri kwa polisi kuandika kazi zao nje ya ofisi yao kwani inasababisha
taarifa nyingi kujulikana au kuvuja kwa siri za kazi ila kupitia msaada huo
tatizo hilo litakuwa limefikia ukingoni kupitia vifaa hivyo.
Mkuu
wa kituo cha polisi Mirerani, mrakibu msaidizi wa polisi (ASP) Evarest Makalla
akizungumza wakati akipokea msaada huo, alisema umetolewa wakati muafaka kwani
utawasaidia kuweka usiri kwenye shughuli zao za kila siku.
Makalla
alisema anaishukuru kampuni ya TanzaniteOne kwa kuwapa msaada wa vitendea kazi
hivyo kwani baada ya yeye kufika kituoni hapo Julai 20 mwaka 2016 alibaini
upungufu wa vifaa hivyo kwani kunasababisha uvujaji wa siri zao.
Alisema
hiyo siyo mara ya kwanza kwa kampuni ya TanzaniteOne kutoa msaada kwa kituo cha
polisi kwani wamekuwa wanawezesha misaada mingine ikiwemo kuweka mafuta kwenye
magari ya polisi pindi wanapofanya shughuli za ulinzi.
“Kupitia
nafasi hii naomba wadau wengine hasa wachimbaji wa madini ya Tanzanite wa vitalu
vingine waige mfano huo kwa kusaidia kituo cha polisi ambacho kinaweka ulinzi
kwa watu wote walipo eneo hilo.” alisema Makalla.
Alitoa
ombi kwa kampuni hiyo ya TanzaniteOne kuendelea kutoa msaada kwenye kituo hicho
kwani bado wana changamoto ya ukosefu wa pikipiki zitakazowawezesha kuendeleza
ulinzi vizuri kwenye eneo hilo.
Meneja
wa ulinzi wa kampuni ya TanzaniteOne, Abubakary Lombe alisema kampuni hiyo
itaendelea kushirikiana na askari polisi wa kituo hicho kwani wamekuwa ni wadau
wao wakubwa kwenye suala zima la ulinzi wa eneo hilo.
“Baada
ya msaada huu wa vifaa vya ofisini, hatujafunga mlango wa kusaidiana kwani wote
tunategemeana na pia suala la ulinzi ni mtambuka, hivyo tutaendelea kuwa pamoja
kwa ajili ya faida yetu sote,” alisema Lombe.


0 Comments