Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema
Nchimbi (wa pili kulia) akishiriki kuvua samaki aina ya kambare kwenye bwawa
lililopo kwenye shamba la samaki la Mikumbi mjini hapa ikiwa ni sehemu ya
uzinduzi uvuvi kwenye shamba hilo.
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema
Nchimbi (wa kwanza kulia) akitoa maelekezo kwa mmiliki wa shamba la ufugaji
samaki la Mikumbi Bw. Charles Kidua (wa pili kulia) wakati akikagua shamba hilo
lenye mabwawa sita yaliyofungwa samaki aina ya sato na kambare.
Mmiliki wa shamba la samaki Mikumbi
mjini Singida na afisa maliasili Mkoa wa Singida Charles Kidua (aliyenyoosha
mkono) akimweleza jambo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi (wa kwanza
kulia) muda mfupi kabla ya kuzinduliwa kwa uvuvi kwenye shamba hilo asubuhi ya
leo.
Baadhi ya samaki aina ya kambare
waliovuliwa mapema leo kwenye uzinduzi wa uvuvi shamba la samaki la Mikumbi
lililopo mjini hapa.
.........
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema
Nchimbi ameziagiza halmshauri zote za Mkoa wa Singida kuanzisha mabwawa
ya ufugaji wa samaki ili kutunza mazingira, kuongeza kipato na kuwa
darasa la kufundishia vikundi na wananchi wengine.
Dkt.
Nchimbi ametoa agizo hilo mapema asubuhi ya leo katika shamba ya
ufugaji wa samaki la Mikumbi lililopo manispaa ya Singida linalomilikiwa
na Bwana Charles Kidua wakati wa uzinduzi wa mavuno ya kwanza ya samaki
aina ya kambare katika mabwawa matatu kati ya sita yaliyopo katika
shamba hilo.
Amesema halmashauri
zionyeshe mfano kwa kuiga mbinu ya ufugaji wa samaki katika kutunza
mazingira kwakuwa itaongeza kipato cha halmashauri pia halmashauri
iangalie namna ya kufundisha ufugaji wa samaki vikundi vya vijana kuliko
kuwapa mikopo ya pesa ambayo huishia kutumika vibaya.
Dkt.
Nchimbi ameongeza kuwa uwepo wa mabwawa hayo ya ufugaji wa samaki
unaonyesha kuwa Mkoa wa Singida sio kame na wala sio mkoa masikini na
uko tayari kuandaa chakula kulisha mikoa ya jirani hasa makao makuu ya
nchi ambayo ni Dodoma.
“Tumejipanga
na tuko vizuri kuhakikisha Dodoma inapata chakula kizuri na cha uhakika,
Singida sio kame wala masikini, samaki hawafugwi kwenye ukame, Singida
sio kame hata kidogo” amesisitiza Dkt. Nchimbi.
Ameongeza
kuwa watendaji wote wanapaswa kuziishi taaluma zao kama ambavyo mmiliki
wa mabwawa hayo ambaye ni afisa maliasili ambaye ameweza kuanzisha
bwawa la samaki na hivyo kuwataka watendaji wengine mfano maafisa
kilimo, mifugo kuwa mifano kwa jamii kwa kuonyesha manufaa ya taaluma
hizo.
Naye mmiliki wa mabwawa hayo
Bw. Charles Kidua amesema amekuwa na wazo la kuanzisha mabwawa ya
ufugaji wa samaki kwa muda mrefu lakini amefanikiwa kuanzisha mradi huo
mwaka 2016 kwa gharama ya shilingi milioni 12.
Kidua
amesema kuanzishwa kwa mabwawa hayo kumewafaidisha baadhi ya wananchi
amabo tayari wamejifunza kutka kwake na kuchukua vifaranga vya samaki
kwake.
“Ukiwa na eneo zuri lenye maji
uanzishaji wa ufugaji wa samaki kwa bwawa moja unaweza kukugharimu
shilingi laki tatu tu, jirani yangu hapa yeye ameanzisha bwawa lake na
kuchukua vifaranga hapa kwangu, kuna wananchi wengine pia wameanzisha
mabwawa yao kupitia elimu wanayojifunza kutoka hapa” amesema Kidua.
Ameongeza
kuwa changamoto aliyokumbana nayo katika kuanzisha mradi huo ni pamoja
na ukosefu wa vifaranga wa samaki katika mikoa jirani na hivyo kumlazimu
kuvifuata Mwanza hali ambayo inaongeza gharama.
Baadhi
ya maofisa wa serikali na wananchi walioshuhudia uvunaji wa samaki hao
wamekiri kuhamasika na wao kuanzisha ufugaji wa samaki. Mavuno ya samaki
aina ya kambare katika shamba hilo yatafuatiwa na uvunaji wa samaki
wengine aina ya sato ambao pia wapo katika mabwawa ya shamba hilohilo.




0 Comments