Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba
akiwasikiliza wakazi wa Kata ya Uchunga alipokwenda kufanya ziara na kuwatahadharisha
kuhusu uvamizi wa ndege waharibifu wa mazao, kwelea kwelea.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba (mwenye
trakisuti ya bluu) akizungumza na watoto katika Shule ya Msingi Balele iliyopo
Kata ya Mwadui Lohumbo alipokwenda kuwapa elimu kuhusu uaharibu wa ndege kwelea
kwelea. Pembeni yake ni Mkuu Afisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika, George
Kessy.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba
akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nyenze Kata ya Idukilo.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba akiwapungia mikono wakulima waliokuwa wakiendelea na shughuli shambani katika Kata ya Mwadui Lohumbo.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba
akizungumza na wananchi wa eneo la Utemini Kata ya Mwadui Lohumbo alipokuwa
akiwatembelea na kuwatahadharisha kuhusu uvamizi wa ndege waharobifu mazao
kwelea kwelea.
Na Mwandishi Maalumu, Kishapu
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Nyabaganga
Taraba amewataka wananchi wilayani humo kuchukua tahadhari na baa la ndege
waharibifu wa mazao mashambani aina ya kwelea.
Amesema tayari baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo yamevamiwa
na ndege hao waharibifu wa mazao yakiwemo ya mtama, uwele, alizeti na mahindi
yanayoanza kustawi.
Taraba ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na
Usalama alitoa tahadhari hiyo kwa wananchi mwishoni mwa wiki alipofanya ziara ya
katika vijiji vya kata sita zilizopo wilayani humo.
Akiwa amembatana na Ofisa Kilimo, Ushirika na
Umwagiliaji Wilaya, George Kessy na Ofisa Nyuki na Mkuu wa Jeshi la Polisi
Wilaya (OCD), Emmanuel Gariyamoshi aliwatembelea wananchi wa kata za Uchunga,
Mwadui Lohumbo, Idukilo, Ukenyenge, Mwamasele na Mwaweja.
Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kulinda mashamba
yao na kuwafukuza ndege hao wakati Serikali inaendelea kuchukua hatua za haraka
ili kuwasaidia.
Alisema tayari wilaya imeagiza ndege maalumu kwa ajili
ya kumwaga sumu kwenye mazalia ya ndege hao ili wasiongezeke na kuleta madhara
zaidi kwa mashamba ya wananchi.
“Serikali haijawatupa nawaomba wananchi tukae
mashambani mwetu tulinde na kuwafukuza ndege hao wasile mazao yetu kwani
tutapata hasara kubwa, hatujui hao kwelea kwelea watakuja lini, na hatujui hiyo
ndege itakuja lini,” alisisitiza.
Aidha, aliwataka wananchi kuvuna haraka iwezekanavyo
mazao ambayo tayari yamekomaa ili kutowapa mwanya ndege hao kufanya uharibifu
wao na hivyo kuwapa hasara wakulima.
Aliwataka wakulima wasihadaiwe na kuuza mazao yote kwa
wafanyabiashara hali inayoweza kuwasababishia kukosa chakula baadaye na kulazimika
kununua chakula kwa bei ya juu.
Aliwaonya watu wanaofanya hivyo kwani huwaacha nyuma
wakulima waliotoka jasho kulima mazao wakati wao wakineemeka kwa kuyauza mazao
hayo kwa bei ya juu na kupata faida.
Kwa upande wake, Kessy alisema idara yake
inawasisitizia wananchi wajenge utamaduni wa kuhifadhi chakula cha kutosha
ghalani ili kiwasaidia katika siku zijazo na kuuza tu ile ziada inayobaki baada
ya kutosheka.
Aliwapa mbinu za kufukuza kwelea kwelea kwa kuweka
vitambaa mithili ya bendera, sanamu za watu na kupiga madebe ili kuwafukuza
ndege hao ili wapiti mbali ya mashamba wasiweze kufanya uharibu.






0 Comments