Random Posts

SEKTA YA MAWASILIANO NGUZO MUHIMU YA UKUAJI WA UCHUMI

Benjamin Sawe Maelezo

TANZANIA kama ilivyo nchi zingine duniani, imeshuhudia ukuaji wa sekta ya mawasiliano ambayo imechangia katika kuboresha maisha ya wananchi kijamii na kiuchumi sambamba na pato la taifa.

Ukuaji wa sekta hii umechangiwa na kuwepo kwa sera, sheria kanuni na mfumo mzuri wa utoaji leseni za huduma za mawasiliano.

Sekta hii inachangia katika uchumi moja kwa moja na kwa kupitia sekta ya elimu, afya, kilimo, biashara, ajira, mabenki, utalii, uwekezaji na sekta nyingine zote kama nyenzo ya uwezeshaji katika kuongeza ufanisi wa utendaji kupitia jamii habari.

Takwimu zinaonesha kuwa laini za simu zinazotumika zimeongezeka kutoka 34,251,801 mwaka 2014 hadi kufikia laini 39,808,419 mwaka 2015 na idadi ya watumiaji wa intaneti waliongezeka kutoka 14,217,311 kwa mwaka 2014 hadi kufikia  17,263,523 kwa  mwaka 2015.

Aidha, zaidi ya asilimia 64 ya kaya nchini zinamiliki simu za mikononi. Pia ukuaji huu umeongezeka hadi kwenye vituo vya kurusha matangazo.

Vituo vya kurusha matangazo  ya redio vimeongezeka kutoka vituo 91 mwaka 2014 hadi kufikia vituo 116 mwaka 2015. Wakati Tanganyika inapata uhuru mwak 1961 kulikuwepo na kituo kimoja cha redio kwa sasa ni zaidi ya 140, kituo cha luninga hakikuwepo hata kimoja lakini miaka 55 baadae vipo zaidi ya 25. 

Vilevile, zaidi ya asilimia 79 ya teledensity/penetration rate ambacho ni kiasi ambacho wananchi wamefikiwa na huduma za mawasiliano ikiwemo ya simu, intaneti na utangazaji ambapo watoa huduma za mawasiliano ya simu na posta pia wameongezeka na kuleta ushindani wenye tija na ufanisi nchini kwa sekta zote.

Mafanikio hayo yamewezesha kukua kwa kasi kwa sekta ya mawasiliano kutoka asilimia 8.0 mwaka 2014 hadi kufikia asilimia 12.1 mwaka 2015 na hivyo kuwa sekta ya kwanza katika sekta za huduma na kuwa ya pili kwa sekta zote  katika ukuaji hapa nchini.

Sekta hii imechangia katika Pato Ghafi la Taifa kwa asilimia 3.6 mwaka 2015. Matokeo haya ya ukuaji na mchango katika teknolojia ya habari na mawasiliano kwa sehemu kubwa kumetokana na kuongezeka kwa matumizi ya huduma za mawasiliano zikiwemo zile za muda wa maongezi kwa simu za viganjani na mezani, intaneti na utangazaji.

Pia, ufanisi huu umechangiwa na kukua kwa matumizi ya miamala ya kielektroniki ambayo ni pamoja na uuzaji na ununuzi wa bidhaa na utoaji wa huduma kwa njia za kielektroniki kama vile kutuma na kupokea pesa, kulipia ankara za maji, umeme, ada, leseni za magari na usajili wa makampuni.

Utafiti kupitia tathmini ya Global Microscope umebaini kuwa Tanzania imeshika nafasi ya sita kati ya nchi 55 ulimwenguni na inaongoza katika Bara la Afrika kwa kuwa na mazingira mazuri ya huduma za kifedha kupitia simu za kiganjani.

Vilevile, kwa mujibu wa ripoti ya Fiscope Survey ya mwaka 2015, huduma za kifedha zimewafikia Watanzania kwa asilimia 76 kutoka asilimia 44 mwaka 2009 ikiwa imechangiwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa Mawakala wa Kibenki (Agent Bankings) pamoja na huduma za kifedha kupitia makampuni ya simu kiasi cha kufikia akauti za miamala ya kifedha (mobile money accounts) kuwa 17,639,349 hadi Desemba 2015.

Tanzania ni nchi ya kwanza duniani kwa kampuni za simu za viganjani kuwa na utayari na makubaliano ya kutengamanisha (interoperability) miamala ya huduma ya fedha.

Hii imewezesha kupunguza gharama za kutuma fedha kutoka mtandao mmoja kwenda mitandao mingine. Jambo hili limewezesha Tanzania kuongoza duniani katika kutumia huduma ya Mobile Money Banking kwa kiasi cha fedha zinazozunguka kwenye mtandao kwa wastani wa Shilingi trilioni 4.5 kwa mwezi.

Ukuaji imara na wa kasi wa sekta ya mawasiliano nchini ni sehemu ya matunda yanayoonekana na Serikali.Aidha Sera nzuri za serikali na kufunguliwa kwa soko huria zimewezesha kuongezeka kwa wawekezaji na hivyo kuwapa watumiaji fursa ya kuchagua huduma bora wanayohitaji kwa gharama wanazomudu.

Katika kukabiliana na changamoto ya idadi ndogo ya wananchi wanaotumia huduma za simu, Serikali inaendelea kujenga mkongo wa taifa unaotarajiwa kufikia mikoa yote ili wananchi wote waweze kutumia huduma ya intaneti kwa maendeleo yao.

Profesa Mbarawa anasema wakati Serikali inaanza ujenzi wa mkongo huo ulikuwa umejengwa kiasi cha kilometa 700 lakini hadi leo tayari ujenzi wake umefikia takribani kilometa 18,000.
“Nina uhakika baada ya miaka miwili utakuwa umefikia zaidi ya kilometa 25, 000,” anasema. Anaeleza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa matumizi hayo ya simu nchini na ndio maana imeanzisha huduma za kilimo mtandao, afya mtandao na elimu mtandao ili wananchi na wao waweze kufanikisha mikakati ya kila sekta kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Aidha, maendeleo ya mkongo wa Taifa nchini Tanzania pia umesababisha kuongezeka kwa ukuaji wa uchumi, kupunguza gharama za mawasiliano kutoka dola 20,000 za Kimarekani kwa mwezi hadi dola 160 kwa mwezi, hilo likiwa ni punguzo la asilimia 99.

Pia imepunguza gharama kwa watumiaji wa mwisho kutoka dola 0.06 kwa dakika mwaka 2009 hadi 0.03 dola kwa dakika mwaka 2013 na pia kupunguza gharama za intaneti kutoka dola 16.45 kwa gigabyte moja mwaka 2009 hadi dola 4.11 mwaka 2013.

Hayo ni kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na, na Mawasiliano, Injinia Edwin Ngonyani wakati wa uzinduzi wa Sera ya Mkongo wa Taifa mwaka 2016.

Bwana Ngonyani pia anabainisha kuwa sekta ya TEHAMA ni moja ya nguzo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa taifa kwani ina mchango wa moja kwa moja na pia kwa sekta nyingine.

Wadau wengine waliozungumza wakati wa uzinduzi huo waliipongeza serikali ya Tanzania kwa hatua hiyo kubwa, wakisema itaongeza uwekezaji kwenye sekta ya hiyo nchini humo.

Mshauri wa kiuchumi kwenye Ubalozi wa Finland nchini humo Bwana Oskar Kass anasema upatikanaji wa habari ni haki muhimu kwa raia wote, hivyo sera mpya inapaswa kuzingatia hilo.

Anaipongeza serikali ya Tanzania kwa kusaidia sekta ya kibinafsi ili kuleta huduma za TEHAMA kwa gharama nafuu na kuitaka sekta hiyo kusoma vyema sera mpya ili kujinufaisha na fursa za uwekezaji zilizopo na zitakazoibuka.

Wakati tunapata Uhuru kulikuwa hamna inteneti kipindi cha wakoloni simu zilitumiwa na wamissionari pamoja na maeneo yenye vyombo vya ulinzi na usalama lakini leo kuna watanzania zaidi ya milioni 20 wanaotumia simu za mkoni, kila ofisi ina simu za ofisini,kuna inteneti kila jiji,miji na manispaa,kwa sasa mtoto wa miaka sita anajua kutumia simu.


Ni ukweli usiopingika kuwa sekta ya mawasiliano imekuwa kwa kasi katika ambapo inakadria kukua zaidi ifikapo 2025. Ukuajia wa sekta hii unaenda sanjari na ukuajia wa uchumi kwani mawasiliano bora na injini ya uchumi.

Post a Comment

0 Comments