Na Daudi
Manongi-MAELEZO.
Serikali
kupitia Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto imeanza
hatua za awali za uainishaji wa gharama,uandaaji wa mfumo mbadala na
upembuzi wa kina wa aina ya ubia ili kushirikiana na Sekta binafsi
katika
utoaji wa huduma za uchunguzi wa magonjwa.
Hayo yamesemwa
leo bungeni na Naibu Waziri, Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na
Watoto Mhe.Hamis Kigwangalla wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge Mjini
Dodoma.
“Kufuatia
kukua kwa kasi kwa Sayansi na Teknolojia ya uchunguzi wa magonjwa,Wizara
inakubaliana na wazo hili juu ya kuangalia namna nzuri ya kushirikiana na sekta
binafsi katika utoaji wa huduma hizi,”Alisema Mhe.Kigwangalla.
Amesema kwa
kuanzia sasa Wizara yake inafikiria kuanzisha ushirikiano kwa kupitia
ukodishaji wa vifaa ambapo Serikali itakodisha mashine hizo ambazo zitakuwa za
mbia na Serikali haitahusika na ununuzi,ufungaji na matengenezo kinga ya
mashine hizo.
Aidha amebainisha
kuwa katika mfumo huo,Wizara itakuwa na jukumu la kusimamia utoaji wa huduma na
itapata gawio lake kutokana na makusanyo yatokanayo na uchangiaji wa huduma
kulingana na mkataba.
“Ni imani ya Wizara
kuwa kutumia mfumo wa ubia na sekta binafsi(PPP) huduma za uchunguzi wa
magonjwa zitaimarika na kuipunguzia Serikali mzigo wa gharama”,Aliongeza
Mhe.Kigwangalla.

0 Comments